WARAKA WA DAVID KAFULILA KWENDA KWA MAGUFULI - Rhevan Media

WARAKA WA DAVID KAFULILA KWENDA KWA MAGUFULI

Hatimaye imekuwa! Vinara katika ufisadi wa IPTL/ESCROW Singasinga Seth na Rugemarila watiwa nguvuni. Huu ni uamuzi mkubwa uliosubiriwa sana. Na siku zote sikujua kwanini Mhe Rais alikuwa anahofu kuagiza hatua hii.

Sikujua kwanini, kwasababu wakati wa mnyukano wa hoja hii, Mhe Rais alikuwa bungeni na alikuwa sehemu ya maazimio ya Bunge kutaka mitambo ya IPTL itaifishwe na wahusika watiwe nguvuni..

Nakumbuka nikiwa kwenye kipindi kigumu hata kutishwa kuondolewa kichwa na kuitwa majina ya wanyama, yeye alikuwa miongoni mwa mawaziri 5, walionidokeza kwamba ESCROW ni dili nikomae tu mpaka kieleweke!

Nampongeza Mhe Rais kwa uamuzi huu muhimu uliosubiriwa siku nyingi kuamua hatma ya ufisadi huu uliomshinda vibaya mtangulizi wake.

Singasinga huyu alinifungulia kesi kunidai Sh300bn Mahakama Kuu ya Tanzania mwaka 2014, Agust2015 nikamshinda lakini akaamua kunifungulia upya Mahakama ya Kisutu akidai Sh100m, zote akidai nimsafishe kuwa yeye na wenzake hawakuchota zaidi ya 300bn kifisadi.

Kifupi naomba PCCB na DPP wasituangushe watanzania. Nilipata kuwaza kumwomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali anipe kibali niendeshe kesi na hawa majabali wa escrow kwani nina ushahidi wakutosha,Sasa nina furaha kwamba PCCB wameamua kuwaburuza.

Nashauri mambo machache;
1.Mali zote za wahusika hawa ziwekwe chini ya ulinzi kabla hawajahamisha umiliki kwani ni muhimu zikakamatwa kusubiri hukumu ya kesi hii ya Tanzania lakini pia kesi iliyopo Mahakama ya kimataifa ya International Centre For Settlement of Investment Disputes (ICSID). Ambako Septemba 2016, iliamuliwa tulipe Bank ya SCB-HK kiasi zaidi ya 400bn kwa kuwa ndio wamiliki halali wa IPTL na wenye share certificate za IPTL..

Mwaka huu TANESCO imekata rufaa. Najua TANESCO hawajakata rufaa kushinda kesi bali kuomba wapunguziwe hukumu ifanane na uamuzi wa ICSID wa Feb 2014.

Lakini kwakuwa Singasinga Seth alisaini hati na Benki Kuu ya Tanzania, kwamba deni lolote lotakalotokana na migogoro ya IPTL atawajibika yeye na wenzake wanaomiliki kampuni PAP, ndio maana nasisitiza Mali za watu hawa zishikiliwe.

2. Mtambo wa IPTL uwekwe chini ya TANESCO kama ilivoazimiwa na Bunge Nov 2014, tuachane kabisa na kulipa matapeli 7bn kila mwezi ambazo ni malipo ya capacity charges walizokuwa wanalipwa na serikali hii bila kujali IPTL imezalisha au haijazalisha umeme.

3. Mwisho watanzania watambue kwamba huyu Singasinga anaetambulishwa kama mmiliki wa PAP iliyopora 300bn za escrow kama mmiliki mpya wa IPTL, mpaka fedha hizo zinaporwa alikuwa anamiliki asilimia50% tu ya kampuni lakini asilimia 50 zilikuwa zikimilikiwa na kampuni ijulikanayo kama SIMBA TRUST, inayomilikiwa na watu wasiojulikana. Hawajawahi kutajwa popote kwenye report zote.

Nilijaribu kutaka majina yao kwenye Kamati ya Viwanda wakati tukiwahoji BRELA na hata baadae bungeni Serikali iliendelea kusisitiza kuwa majina hayo ni SIRI. Hawa ni wahusika muhimu sana wajulikane kwani inawezekana ndio msingi wa serikali ya awamu ya nne kuibeba IPTL kama mtoto!

Naam, hongera Mhe Rais kwa hatua hii, nazidi kuomba Mungu kesi hizi zifike mwisho kwani kwangu leo ni siku muhimu katika kumbukumbu zangu kuliko Aprili 28, 2015, siku niliyopewa tuzo kwa mapambano dhidi ya ufisadi kwa rejea ya sakata la ESCROW, kwani tuzo haina maana kama vita haifiki mwisho.

Mwisho nishauri asiwepo yeyote wakulindwa kwa Kinga yoyote kwani Katiba na Sheria vipo kwa ajili ya watanzania na sio watanzania kwajili ya Katiba na Sheria. Tusipofika huko vita ya UFISADI mkubwa itakuwa ngumu sana kufika mwisho.

David KAFULILA
JUNE19,2017
Previous
Next Post »