Hivi karibuni Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imezindua programu ya kitaifa ya kukuza ujuzi wa nguvu kazi wa stadi za maisha kwa vijana mkoani Iringa ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/2017 hadi 2020/2021.
Akiwasilisha hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge 2017/2018 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) alisema kuwa kwa kutambua kuwa asilimia 56 ya nguvu kazi ya taifa ni vijana, ndiyo maana imechukua jukumu la kutekeleza programu ya kukuza ujuzi na stadi za kazi kwa vijana.
Madhumuni ya programu hiyo ni kuwawezesha vijana kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda pamoja na kuinua ari ya vijana kupenda kufanya kazi ili kuwaongezea kipato na kuinua hali zao za maisha.
Awamu ya kwanza ya programu hiyo itawanufaisha vijana wapatao 3,400 ambao watapata mafunzo ya stadi mbalimbali ambazo zitawasaidia kujiajiri na kuajiriwa na hatimaye kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa taifa.
Akifungua mafunzo hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama alisema kuwa program hiyo inagharimiwa na Serikali ya awamu ya tano kwa kushirikiana na Taasisi ya Wasalesiani wa Don Bosco.
Alisema kuwa Serikali haitasita kusitisha mkataba na taasisi hiyo endapo watagundua kuwa mafunzo yanayotolewa hayatakuwa na viwango na ubora wanaohitaji.
Naye Padre Simon Akira aliahidi kuwa watafanya vizuri na aliishukuru Serikali kwa kuatambua mchango wa taasisi hiyo wa kuwahudumia vijana.
“Mpango huu ni sehemu ya kuwaandaa vijana ambao watashiriki katika mapinduzi ya viwanda nchini na utasaidia kutoa fursa kwa vijana kupata mafunzo ya uanagenzi katika nyanja za ujenzi, TEHAMA, ufundi magari na ushonaji nguo” alisema Mhe. Mhagama.
Aidha, alisema kuwa Serikali imeweka mipango mbalimbali ya kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. Kwa sasa mwelekeo wa miaka mitano 2016 hadi 2021 ni kujenga taifa lenye viwanda vya kuzalisha biashara za kutosheleza mahitaji ya soko la ndani na kuuza nje ya nchi.
Ili kufikia azma hiyo, nguvukazi yenye ujuzi wa kutosha kumudu mahitaji ya soko la ajira ni muhimu iwepo.
Kutokana na umuhimu huo, Serikali ilijumuisha programu hiyo ili kukuza ujuzi na nguvu kazi ya taifa hususani vijana ili pamoja na kupata ujuzi ipunguze tatizo la ajira nchini. Programu hiyo ya miaka mitano inahusisha vijana kutoka mikoa yote nchini.
Katika utafiti wa nguvu kazi uliofanyika 2014, unaonesha idadi kubwa ya nguvu kazi iliyokuwa kwenye ajira takribani asilimia 79.9 ina kiwango cha chini cha ujuzi na asilimia 16.6 ina kiwango cha kati cha ujuzi ambapo asilimia 3.6 ina kiwango cha juu cha ujuzi.
“Ili kutufikisha katika uchumi wa kipato cha kati, taifa linatakiwa kuwa angalau na asilimia 12 ya ujuzi wa kiwango cha juu, asilimia 34 ya ujuzi wa kiwango cha kati na kutozidi asilimia 54 kwa kiwango cha chini “ alisema Mhe. Mhagama.
Katika kuhakikisha mpango wa maendeleo wa miaka mitano kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021 , Serikali kupitia programu hiyo inalenga ifikapo mwaka 2021 vijana wapatao 100,000 wapate mafunzo kupitia programu za uanagenzi, kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu 1,200,000 na kutoa mafunzo ya kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi 1,700,000.
Aidha, programu hiyo itatambua na kurasimisha ujuzi uliopatikana wa vijana 1,000,000 walioajiriwa na waliojiajiri ili kuziba nafasi hiyo ya ujuzi.
Mafunzo hayo pia ni maandalizi ya kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na vijana wengi wenye sifa na stadi za kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo viatu na nguo ili kuhakikisha nchi inakuwa mstari wa mbele katika kutimiza makubaliano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo ni kuachana na nguo na viatu vya mitumba ifikapo 2018.
Mafunzo hayo pia yanalenga kuwaandaa vijana wengi wenye stadi mbalimbali na kuhakikisha kuwa wanawezeshwa kufanya kazi katika viwanda vilivyopo na vitakavyojengwa.
Kwa upande wa sekta ya nguo na viatu, vijana 3,000 wameanza kupata mafunzo kwa kubuni na kushona nguo kwa kutumia teknolojia za kisasa kupitia kiwanda cha TOOKU kilichopo jijini Dar es salaam na kiwanda cha MAZAVA cha mjini Morogoro.
Vijana wengine watapata mafunzo ya kutengeneza bidhaa za ngozi ikiwemo viatu na pochi, uselemala, ufundi uashi, ufundi magari, uchongaji vipuri, ufundi bomba, ufundi vyuma na kuweka terazo na vigae.
Hakika taasisi ya Net Don Bosco Tanzania kupitia Vyuo vyake nane nchini vitahusika kuwapatia mafunzo vijana wengi zaidi nchini ili waweze kutoa mchango wao kwa familia zao na taifa kwa ujumla.
Naye Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa programu hiyo ya miaka mitano ndiyo fursa ya ajira pekee ya kumfanya kijana aweze kujiajiri na kuajiri vijana wenzake.
Waziri Mhagama alitoa wito kwa viwanda na taasisi mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushirikiana na Serikali katika kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo kwa vijana hao ili kuwajengea umahiri wa stadi za kazi ili kuwawezesha vijana wenye ujuzi bora kuajiriwa na kuwaajiri watakapohitajika.
Fursa hiyo adhimu kwa Vijana ni muhimu, wanapaswa kuitumia kama njia itakayowapa mtaji waweze kujifunza stadi mbalimbali na baadaye waunde vikundi na kufungua kampuni na viwanda vidogo vidogo vya kutengeneza bidhaa mbalimbali.
Sign up here with your email