Mkurugenzi wa Miradi kutoka shirika la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI) Dk. Safila Telatela akizungumza wakati wa kufungua Ariel Camp (Kambi ya Ariel) ya siku tano kuanzia June 19,2017 – June 23,2017 iliyokutanisha watoto na vijana 50 kutoka mikoa ya Shinyanga,Mwanza na Geita jijini Mwanza.Picha na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Mratibu wa Ukimwi wa Mkoa wa Mwanza Dk. Pius Maselle akifungua kambi ya watoto na vijana ‘Ariel Camp’ katika hotel ya Lesa Garden jijini Mwanza.Wa kwanza kushoto ni Mratibu wa Miradi AGPAHI mkoa wa Shinyanga,Dk. Gastor Njau akifuatiwa na Mratibu wa Ukimwi mkoa wa Geita Dk. Joseph Odero. Wa kwanza kulia ni Mratibu wa Miradi AGPAHI mkoa wa Mwanza, Olympia Laswai akifuatiwa na Mkurugenzi wa Miradi AGPAHI, Dk. Safila Telatela.
*****
Jumla ya watoto 8,615 kutoka mikoa ya Tanga, Mara, Mwanza,Geita, Simiyu na Shinyanga wamepatiwa huduma za Virusi vya Ukimwi na Ukimwi ikiwemo kupatiwa dawa za kupunguza makali ya VVU (ARVs) katika kipindi cha kuanzia mwaka 2011 hadi mwezi Machi 2017.
Huduma hizo zimetolewa na shirika la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI) linalojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto.
Takwimu hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa Miradi kutoka AGPAHI,Dk. Safila Telatela wakati wa kufungua Kambi ya Ariel ‘Ariel Camp’ ya siku tano inayokutanisha watoto na vijana wenye umri kuanzia miaka 10 mpaka 17 kutoka mikoa ya Shinyanga,Geita na Mwanza inayofanyika katika Hotel ya Lesa Garden jijini Mwanza.
Dk. Telatela alisema watoto hao ni sawa na asilimia 5 kutoka jumla ya watu 189,806 waliopatiwa huduma na shirika hilo katika kipindi hicho na shirika linaendelea na kazi ya kutoa matunzo na tiba za VVU katika vituo 553 katika mikoa hiyo sita.
Alisema pia wanafanya kazi ya kutokomeza maambukizi ya VVU kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto katika vituo 631.
Aidha Dk. Telatela alisema wamefanikiwa kuunda vikundi zaidi ya 65 vya watoto na vijana katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu ambapo takribani watoto 2640 wamenufaika na vikundi hivyo.
“Kuanzia mwezi Oktoba 2016, shirika letu limeongeza wigo wa kutoa huduma kutoka mikoa miwili ya Shinyanga na Simiyu na sasa imekuwa sita na tunafanya kazi ya kutoa matunzo na tiba za VVU katika vituo 553 kwenye mikoa hii sita”,alieleza Dk. Telatela.
“Shirika letu limekuwa likiandaa kambi kwa ajili ya watoto na vijana kwa lengo la kuwakutanisha ili kujifunza mambo mbalimbali kuhusu afya, stadi za maisha, kupata ushauri wa kisaikolojia kutokana na changamoto wanazokutana nazo na pia huduma za kitabibu kutoka kwa daktari wa watoto katika kipindi chote cha kambi na kuwafanya kuwa mabalozi wa huduma za watoto katika jamii zao”,aliongeza.
Naye Mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa kambi hiyo, Mratibu wa Ukimwi wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Pius Maselle alitoa rai kwa mikoa mipya ya AGPAHI (Geita,Tanga,Mara na Mwanza) kufanya jitihada za ziada katika uundaji wa vikundi vya watoto na vijana ili idadi ya watoto watakaonufaika na huduma za kisaikolojia iwe kubwa.
Aidha Dk. Maselle alitoa shukrani kwa shirika la AGPAHI kwa jitihada mbalimbali linazofanya katika mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi nchini kwa ufadhili wa Watu wa Marekani kupitia shirika la Centres for Disease Control and Preventation (CDC),mfuko wa kusaidia Watoto wenye VVU Kwa hisani ya watu wa Uingereza (CIFF) na Shirika la Development Aid From People to People (ADPP – Mozambique).
HII HAPA HOTUBA FUPI YA UFUNGUZI WA KAMBI YA WATOTO NA VIJANA (ARIEL CAMP) 2017 ILIYOTOLEWA NA MKURUGENZI WA MIRADI AGPAHI,DR. SAFILA TELATELA
Ndugu,
· Mgeni rasmi – Mratibu wa Ukimwi wa Mkoa wa Mwanza,
· Mratibu wa Ukimwi wa Mkoa wa Geita,
· Wafanyakazi wa AGPAHI,
· Watumishi wa afya walioambatana na watoto (walezi wa watoto)
· Watoto wa Kambi ya Ariel,
· Waandishi wa Habari,
· Mabibi na Mabwana.
Habarini za asubuhi!
Awali ya yoye, napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha wageni wote katika hafla hii fupi ya ufunguzi wa kambi yetu ya nane (8) tangu kuanzishwa kwa shirika la AGPAHI mwaka 2011. Pia napenda kutoa shukrani kwenu wote kwa kujumuika na sisi hapa siku hii ya leo, Asanteni sana!
Nichukue fursa hii kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa shirika la AGPAHI kuwashukuru wafanyakazi wenzangu wa AGPAHI na walezi wa watoto kutoka Geita, Shinyanga na Mwanza kwa kushiriki katika kuandaa kambi hii tangu hatua za awali za kuwachagua watoto na vijana huko vituoni kwao, kuwasafirisha na kuwafikisha hapa Lesa Garden – Mwanza. Hongereni sana na Mungu awabariki!
Ndugu mgeni rasmi, napenda kutoa shukrani kwa Watu wa Marekani kupitia shirika lao la CDC ambao ndio wahisani wa kambi hii. Hata hivyo tuna wafadhili wetu wengine wa miradi kama vile Children Investment Fund Foundation (CIFF) and Development aid from People to People (ADPP – Mozambique). Tunawashukuru sana.
Ndugu mgeni rasmi,Shirika la AGPAHI ni shirika lisilo la kiserikali linaloendeshwa na watanzania na watanzania wenyewe ndio sisi hapa.
Shirika letu lilianzishwa mwaka 2011 kutokana na dira ya serikali ya Tanzania na ile ya wafadhili yaani serikali ya Marekani kutaka wazawa (serikali pamoja na mashirika yasiyo ya serikali) kuendesha miradi mbalimbali inayoshughulikia masuala ya VVU na UKIMWI na masuala ya afya ya mama na mtoto ili kuwa na miradi endelevu.
Kuanzia mwezi Oktoba 2016, shirika letu limeongeza wigo wa kutoa huduma kutoka mikoa 2 hadi sita ambayo ni Tanga, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga. Huduma zitolewazo ni pamoja na tiba na matunzo kwa watu wenye VVU, kuzuia maambukizi ya VVU toka kwa mama kwenda kwa mtoto, uchunguzi wa awali na tiba ya saratani ya shingo ya kizazi na kutoa huduma shirikishi za kifua kikuu na UKIMWI sehemu za migodini.
Takwimu
Ø AGPAHI inafanya kazi ya kutoa matunzo na tiba za VVU katika vituo 553 kwenye mikoa sita (Tanga, Mara, Mwanza,Geita, Simiyu na Shinyanga).
Ø Huduma ya kutokomeza maambukizi ya VVU kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto katika vituo 631.
Ø Kutoa huduma ya uchukuaji wa sampuli ya damu kavu kwa watoto katika vituo 631.
Ø Huduma shirikishi za kifua kikuu na Ukimwi katika maeneo manne (5) ya migodi (Mererani, Iyenze, Mwime, Kalole, Kakola na Mwazimba).
Ø Hadi mwezi Machi 2017, jumla ya watu waliowahi kupata huduma za VVU/Ukimwi ikiwemo kupata dawa za kupunguza makali ya VVU (ARV) ni 189,806 kati yao watoto walikuwa 8615, hii sawa ni asilimia 5%.
Ø AGPAHI pia inatoa huduma mseto za uzazi wa mpango katika vituo vya ushauri nasaha na upimaji wa hiari na tiba na matunzo vinavyowezeshwa na AGPAHI.
Kwa kutambua umuhimu wa watoto na vijana, Shirika la AGPAHI lilianzisha huduma za kisaikolojia kwa kupitia vikundi vya watoto tangu mwaka 2011 pindi lilipoanzishwa (ambapo Shirika lilikuwa linafanya kazi katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu). Huduma hizo zilihusisha uundwaji wa vikundi vya watoto na vijana katika vituo vya kutolea huduma za afya (yaani CTC).
Kwa sababu ya umuhimu wa vikundi hivi, AGPAHI imeshaanza juhudi za makusudi za kuanzisha vikundi kwenye mikoa minne (4) ambayo tumeanza kufanya kazi tangu Oktoba 2016 (Mwanza, Mara, Geita na Tanga). Azma yetu ni kuhakikisha tunawaunganisha watoto na vijana wengi kwenye huduma za kisaikolojia kwa kupitia vikundi.
Kutokana na uundwaji wa vikundi vya huduma za kisaikolojia kwa watoto na vijana, AGPAHI ilifanya juhudi za kuanzisha kambi za watoto ambazo hufanyika mara moja au mbili kwa mwaka. Kambi hii tunayoizindua leo ni kambi ya nane (8) kufanyika chini ya uratibu wa shirika la AGPAHI (kwa mwaka huu hii ni kambi ya pili kufanyika). Kambi nyingine za awali zimeshanyika katika mikoa ya Kilimanjaro, Kagera na Mwanza. Utaratibu huu wa kuwapeleka watoto na vijana kwenye kambi zilizopo maeneo tofauti ni mzuri kwani unasaidia kuwafundisha mambo mengi kuhusu nchi, historia na tamaduni bila kusahau masomo wanayopata wakiwa kambini.
Ndugu mgeni rasmi,
Kambi hii inahusisha watoto na vijana kutoka katika mikoa ya Geita, Shinyanga na Mwanza yenye jumla watoto 50 na watumishi wa afya (walezi wao) 11. Watoto pamoja na watumishi wa afya wametoka katika vituo mbalimbali kama walivyotambulishwa awali. Wana umri kati ya miaka 10 -17.
Washiriki wa kambi wakiwa hapa kambini hufundishwa kuhusu afya na makuzi, lishe, stadi za maisha, elimu sahihi kuhusu VVU na Ukimwi, ufuasi mzuri wa dawa pamoja na unyanyapaa na unaguzi.
Pia hupata ushauri wa kisaikolojia kutokana na changamoto wanazokutana nazo na pia huduma za kitabibu kutoka kwa daktari wa watoto katika kipindi chote cha kambi.
Vilevile, naomba kuchukua fursa hii, kuwasihi watoto na vijana kuzingatia elimu na kanuni za afya kama wanavyoelekezwa na wataalam wa afya na endeleeni kuwa wanachama wazuri katika vikundi vyenu na muwe mabalozi wa kuwahamasisha watoto na vijana wenzenu kujiunga na vikundi.
Mwisho ningependa kuwashukuru watumishi wa afya mliokuja na watoto kutoka Geita, Shinyanga na Mwanza. Nawasihi muendelee kuwajenga na kuwasimamia watoto ili wawe mabalozi wazuri kwa wengine, ili baadae tujivunie ushiriki wao katika kambi ya Ariel 2017.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA!
Sign up here with your email