Dar es Salaam. Wanafunzi wanaosoma vyuo vikuu nchini wamesema wanapenda kufanya kazi zenye nafasi za juu zinazoendana na fani wanazosomea kama vile ukurugenzi, umeneja au uofisa wa kitengo fulani katika kada hiyo.
Utafiti mdogo uliofanywa na gazeti la Mwananchi jana kwa njia ya mahojiano na umehusisha sampuli za wanafuzi 15 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Ardhi na kile cha Tumaini.
Katika utafiti huo wanafunzi 10 kati ya 15 wanapenda kuajiriwa katika nafasi ya kada wanazosome na siyo kujiajiri.
Pia, utafiti umeonyesha kuwa wanafunzi wawili kati ya 15 wanapenda kuajiriwa katika nafasi za juu ili wapate mtaji wa kujiajiri baadaye na watatu wamesema wanapenda kufanya kazi yoyote hata kama ni nje ya kozi walizosomea.
“Napenda kufanya kazi wizara ya ardhi kama ofisa au mkurugenzi fulani hiyo ndiyo ndoto yangu,” amesema Aneth John mwanafunzi wa mwaka wa pili Chuo Kikuu cha Ardhi.
“Napenda nikimaliza masomo yangu ya saikolojia niajiriwe kama mtaalamu wa saikolojia katika moja ya hospitali kubwa nchini,” amesema Janeth Alexander mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayechukua fani ya uhandisi, Simon Kapaya amesema anapenda kujiajiri lakini kabla ya kujiajiri akimaliza masomo atafanya kazi ya nafasi ya juu kama mwajiriwa ilia pate mtaji.
“Sipendi kuajiriwa ila napenda kufanya kazi inayofanana na kozi yangu ili baadaye nije kujiajiri kupitia fani yangu,” amesema.
Furaha Fikiri ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili Chuo Kikuu cha Tumaini anaungana na Kapaya kuwa anatamani kujiajiri, lakini kabla ya kujiari anapenda kufanya katika moja ya ofisi kubwa itakayomsaidia kupata mtaji wa kuja kujiajiri.
Sophia Mussa wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Ardhi anatofautiana na wanafunzi wenzake kwa kusema; “Nikimaliza masomo nitafanya kazi yoyote ile hata ya kuokota makopo ili nipate pesa.”
Anaongeza kuwa, “kazi ni kazi na unaposoma usifikirie kwamba utapata ajira moja kwa moja ,kwa hiyo lazima ujiandae kisaikolojia utakapomaliza masomo uwe tayari kufanya kazi yoyote hata kama iko nje ya fani yako.”
Sign up here with your email