MAZUNGUMZO ya kumaliza mzozo wa mchanga wenye madini (makinikia), baina ya Serikali na Kampuni ya Barrick Gold Corporation kupitia mshirika wake, Acacia, yanaweza kuwa si tu magumu, bali yakachukua muda mrefu kupata suluhisho.
Mazingira hayo yanatokana na uzoefu wa kampuni hiyo katika historia ya kimataifa kuonyesha kwamba inatumia umakini wa hali ya juu kulinda maslahi yake pale panapotokea nafasi ya mazungumzo ya kutafuta suluhisho la jambo lolote linalohusiana na uwekezaji wake katika nchi mbalimbali duniani.
Kwa kutambua changamoto mbalimbali za kiuwekezaji, kampuni hiyo ina bodi maalumu inayohusika na ushauri wa kimataifa ambayo inaundwa na watu wenye ubobezi katika maeneo mbalimbali, hasa ya kisiasa na jiografia.
MTANZANIA Jumamosi limechunguza mwenendo wa kampuni hiyo kuhusu aina ya makubaliano yake ya kiuwekezaji na mataifa mbalimbali na kubaini kuwa imekumbana na misukosuko mikubwa ya uwekezaji wa madini.
Ukiachilia mbali masuala ya makinikia, ambayo kwa sasa yanaipeleka kampuni hiyo kwenye meza moja ya mazungumzo na Serikali, masuala ya mivutano ya ardhi, uchafuzi wa mazingira na migogoro ya mikataba nayo imekuwa ni sehemu ya misukosuko inayoikumba kampuni hiyo katika baadhi ya mataifa ambako imewekeza.
Gazeti hili limebaini kuwa, miongoni mwa mataifa ambayo yanaweza kuchukuliwa kama mfano au Tanzania kujifunza na hata kutafuta mbinu mpya ni Dominica na Saudi Arabia, ambako zilipitia changamoto kama hizi za mikataba mibovu iliyosababisha nchi hizo kunyonywa hadi pale pande zote mbili zilipolazimika kuketi meza moja ya mazungumzo.
Itakumbukwa mapema wiki hii, Rais Dk. John Magufuli baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation, ambaye ni mmiliki mkubwa wa Kampuni ya Acacia Mining Limited, Profesa John Thornton, nchi hizo zilitajwa kwamba zilipita njia kama hii hii inayopitia Tanzania kwa sasa.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kupitia vyombo vya habari vya kimataifa na kwenye mtandao wa intaneti umebaini kuwa, hata ule mgogoro wake wa mkataba wa uchimbaji wa madini na Taifa la Dominica lenye takribani watu milioni 10, mazungumzo ya kutafuta mapatano yalidumu kwa miezi minane.
Inaelezwa kuwa, Serikali ya Dominica iliipa mkataba Kampuni ya Barrick Gold Cooperation wa kuchimba madini kwa miaka 30 katika mgodi wa Pueblo Viejo, ambao ni moja ya migodi mikubwa ya dhahabu duniani.
Katika uwekezaji huo, Kampuni zote mbili ambazo zinatoka nchini Canada, Barrick Gold Cooperation ilimiliki asilimia 60 na Goldcorp asilimia 40.
Msingi wa mgogoro baina ya serikali ya nchi hiyo na Kampuni ya Barrick ni mkataba ambao ulielekeza kuwa nchi hiyo ingenufaika kwa asilimia tatu tu ya faida ya dhahabu inayochimbwa.
Vyombo vya habari nchini Dominica vinaeleza kuwa, vuguvugu la maandamano ya wananchi yasiyokuwa na ukomo ambayo yaliongozwa na asasi mbalimbali za kiraia yaliisukuma serikali ya nchi hiyo kwa kiasi kikubwa kuupitia upya mkataba wake na Kampuni ya Barrick.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo hivyo, baada ya serikali ya nchi hiyo kupitia mkataba upya wa Barrick, iliingia kwenye mazungumzo na kufikia mwafaka wa kulipwa asilimia 28 ya fedha zitokanazo na faida ya dhahabu iliyochimbwa.
Taarifa hizo na zile za Kampuni ya Barrick zinaeleza kuwa; Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 25 kutoka malipo yaliyokuwapo kwenye mkataba wa awali uliokuwa unapigiwa kelele na wananchi.
Tangazo la makubaliano hayo baina ya kampuni hiyo na Serikali ya Dominica ambalo lilitolewa na Barrick Mei 8 mwaka 2013, lilitanabahisha kuwa kusudio la makubaliano hayo ni kuwa na uchumi wenye kunufaisha pande zote mbili.
Katika kutafuta makubaliano hayo, Barrick walipendekeza masharti manne ambayo yalijenga msingi wa kupatikana kwa suluhisho.
Masharti hayo, kwanza ni kuondolewa kwa asilimia 10 ya kodi iliyowekwa kwenye mtaji wa awali wa uwekezaji kwa ajili ya kupata faida (NPI).
Pili, kuongezwa kwa muda ambao utaiwezesha serikali ya nchi hiyo kupitia kampuni yake ya Pueblo Viejo Dominicana Corporation (PVDC) kurejesha mtaji wake uliowekezwa.
Tatu, kusogezwa kwa muda wa kuanza makato mapya yatokanayo na faida (NPI).
Nne, kuwekwa punguzo la kiwango cha makato ya thamani.
Taarifa zinaeleza kuwa, baada ya serikali kukubaliana na mapendekezo hayo, Barrick nayo iliridhia mapendezo ya serikali kwa muktadha wa kuanza kulipa kiwango cha juu cha kodi kilichopendekezwa.
Hata hivyo, ulipaji huo ulianza kufanyika kwa masharti ya kwamba kodi itapandishwa na kushushwa kwa kutegemea bei ya dhahabu kwenye soko.
Pia kiwango cha juu cha makato ya kodi ya dhahabu kitakuwa kinapitiwa na kupangwa upya kila baada ya miaka mitatu kuendana na asilimia 90 ya kodi iliyokuwa inalipwa awali kwenye Kampuni ya Serikali ya PVDC.
Makubaliano hayo yalikadiriwa kuweka usawa wa 50/50 wa mzunguko wa fedha ya madini kati ya Kampuni ya Serikali PVDC na Serikali yenyewe, kati ya mwaka 2013 hadi 2016.
Matokeo yake, Serikali ilitarajia kuvuna zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 2.2 katika kipindi ambacho bei ya dhahabu itakuwa inauzwa kwa dola za Kimarekani 1,600 kwa wakia moja (ounce) ambayo ni sawa na gramu 28.3.
Zaidi faida ya kiuchumi ya mabadiliko hayo yalitarajiwa kufika dola za Kimarekani bilioni 1.5.
Kwa ujumla msingi wa makubaliano mambo matatu yaliafikiwa. Kwanza ni kuongezwa kwa kodi ya mapato kwa asilimia 25, pili mrahaba safi wa makinikia kutozwa kwa asilimia 3.2 na tatu, jumla ya faida yote ya madini kutozwa kodi ya asilimia 28.75.
Mgodi wa Pueblo Vienjo una uhai wa miaka 25 na una madini ya kiwango cha juu na cha chini ambapo kwa mwaka unachangia wastani wa wakia (ounces) 625,000 hadi 675,000 za dhahabu kwa Kampuni ya Barrick.
MKATABA NA SAUDI ARABIA
Taarifa ambazo gazeti hili limezikusanya kutoka katika vyombo vya habari vya Saud Arabia na Kampuni ya Barrick, zinaonyesha kuwa kampuni hiyo mwaka 2014 ililazimika kuingia mkataba wa makubaliano ya uwekezaji wa asilimia 50 kwa 50 na Serikali ya Saudi Arabia kupitia kampuni yake ya madini Ma’aden, kwa ajili ya kuchimba madini ya shaba kwenye mgodi wa Shaba wa Jabal Sayid.
Katika usimamizi au kujua vyote vinavyotoka kwenye uchimbaji huo, mkataba unaipa nafasi Saudi Arabia kusafirisha makinikia ya shaba kwa gharama ya chini.
Kupitia uwekezaji huo, jumla ya pauni milioni 100(kilogramu milioni 45.3) za makinikia ya shaba hupatikana kwa mwaka.
Si hilo tu, mwekezaji huyo mpya atalazimika kufuata misingi yote ya viwango vya maendeleo ya kijamii na kuendeleza kile kinachoitwa ‘Saudization’, yaani kuwaendeleza wazawa katika teknolojia ya uchimbaji madini.
Chini ya makubaliano hayo, pia ni lazima kampuni hiyo iweke asilimia fulani ya nafasi za kazi kwa wananchi wanaozunguka mradi huo na pia kutoa mafunzo maalumu ya utaalamu kwa makampuni ya ndani ya nchi.
Tanzania pia inaweza kuchota uzoefu huu ama kwenda mbali zaidi, hasa wakati ambapo nchi inataka kurekebisha mikataba yake ya madini ambapo inadaiwa nchi inaibiwa sana.
Pamoja na hayo, licha ya kuwa na uzoefu wa changamoto kama hizi katika maeneo inakowekeza, hata hivyo uamuzi huu wa serikali ya Rais Magufuli umeonekana kuiumiza kichwa Kampuni ya Barrick na Acacia kwa ujumla.
Juzi katika kikao cha wanahisa ambacho kilifanyika kwa njia ya simu, kikiongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Acacia, Brad Gordon, kimetoa mwelekeo wa kutaka kujipanga sawasawa kuanzia kwenye kuunda timu ambayo itakuja kufanya mazungumzo hapa nchini.
Miongoni mwa mikakati yao, Acacia imetaka kupata ripoti ya pili iliyowasilishwa kwa Rais Magufuli mapema wiki hii.
Gordon aliwaambia wanahisa hao kuwa ripoti ya kwanza tayari wamekwishaipata na watahakikisha wanaipata ya pili kabla ya kuanza kwa mazungumzo.
Pamoja na hilo, Acacia wametaka kufahamu mapema timu ambayo itaongozwa na Rais Magufuli katika mazungumzo hayo pamoja na namna mazungumzo yatakavyofanyika.
Katika kikao hicho, Ofisa huyo alikuwa makini kueleza moja kwa moja kama wamekubaliana kutekeleza na kile ambacho kimedaiwa katika ripoti hiyo, ikiwamo suala la ujenzi wa kinu cha uchenjuaji wa dhahabu, akisema kuwa suala hilo wameliacha kwenye mazungumzo pindi majadiliano yatakapoanza.
UCHUNGUZI WA TANZANIA KUHUSU MAKINIKIA
Machi mwaka huu serikali ilizuia makontena zaidi ya 200 kwenye Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuchunguza mchanga wa madini (makinikia) ambao ulikuwa unasafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya kuchenjuliwa.
Mchanga huo ulikuwa ni mali ya Kampuni ya Acacia, ambayo ni kampuni mshirika wa Barrick Gold Corporation.
Baada ya zuio la mchanga huo, Rais Dk. John Magufuli aliteua kamati mbili kwa ajili ya kuchunguza makinikia hayo, ambapo kamati ya kwanza iliyokuwa inaundwa na wanasayansi ilibaini kiasi kikubwa cha madini ambayo yangeibiwa kupitia mchanga huo.
Kamati ya pili ya uchunguzi iliundwa na wachumi na wanasheria ambapo ilibaini zaidi ya Sh trilioni 100 zimeibiwa kupitia usafirishaji wa makinikia, huku sheria nyingi za madini zikikutwa na kasoro inayotoa upenyo wa wawekezaji kutorosha madini.
Baada ya ripoti ya pili ya wachumi na wanasheria kuwasilishwa, Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambaye ni mmiliki mkubwa wa Kampuni ya Acacia Mining Limited, wakiwa na hisa asilimia 64, Profesa John Thornton, alikuja nchini na kukutana na Rais, Dk. John Magufuli, ambapo walifanya mazungumzo na kukubaliana kuunda timu mbili za majadiliano.
Timu hizo zitahusisha Serikali ya Tanzania na wawakilishi wa Kampuni ya Barrick kutoka Canada na Marekani na watafanya majadiliano ambayo yatahusu namna ya kufikia mwafaka katika suala la kusafirisha mchanga wa dhahabu (makinikia) nje ya nchi kwa faida ya pande zote mbili.
Sign up here with your email