JAMES Peter, mkazi wa Njiro jijini Arusha, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Arumeru, kwa tuhuma za kubaka watoto wawili.
Peter anatuhumiwa kuwabaka watoto wawili, mmoja akiwa na umri wa miaka minne na mwingine sita.
Katika kesi ya kwanza, mbele ya Hakimu Patricia Kisinda, Wakili wa Serikali, Riziki Maayu, alidai mahakamani hapo jana kuwa katika tarehe tofauti za mwezi Mei, mwaka huu, Peter alimbaka mtoto mwenye umri wa miaka minne (jina linahifadhiwa) katika eneo la Njiro.
Alidai kuwa mtuhumiwa alitenda makosa hayo kinyume cha sheria.
Katika shtaka la pili, Peter anadaiwa katika tarehe tofauti kati ya mwezi Januari na Mei, mwaka huu, katika maeneo ya Njiro alimbaka mtoto mwenye umri wa miaka sita (jina linahifadhiwa).
Mshtakiwa huyo alikana mashtaka hayo na wakili huyo wa Serikali aliieleza mahakama kuwa upelelezi haujakamilika na kuiomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kutaja kesi hizo.
Pamoja na hayo, Hakimu Patricia alimweleza mshtakiwa huyo kuwa dhamana iko wazi chini ya wadhamini wawili ambao ni waajiriwa wa taasisi zinazotambuliwa na mahakama.
Pia, alisema kila mdhamini atatakiwa kusaini dhamana ya Sh milioni 5.
Kesi zote mbili ziliahirishwa hadi Juni 28, mwaka huu zitakapotajwa tena na mshtakiwa alirudishwa mahabusu baada ya wadhamini wake kushindwa kukidhi masharti ya dhamana.
Sign up here with your email