SERA ya elimu bila malipo iliyoanzishwa na Serikali chini ya Rais Dk. John Magufuli, ilisababisha ongezeko la wanafunzi wanalioandikishwa kuanza darasa la kwanza na chekechea na hivyo kusababisha upungufu wa vyumba vya madarasa.
Hata hivyo, miundombinu mingi ya shule za msingi nchini imechakaa hasa kwa shule zilizojengwa zamani ambazo nyingi sakafu zake zimechimbika, majengo kujaa nyufa na madirisha pamoja na milango imeharibika.
Shule ya msingi Itumbi iliyopo katika Kata ya Matundasi wilayani Chunya, Mkoa wa Mbeya, ni miongoni mwa shule zilizokuwa zikikabiliwa na changamoto ya uchakavu wa miundombinu yake hasa vyumba vya madarasa.
Kufuati changamoto hiyo, mchimbaji mdogo wa madini, Edson Kibusu, mkazi wa Kijiji cha Itumbi amejitolea kukarabati vyumba vya madarasa sita na ofisi ya Mwalimu Mkuu
shuleni hapo.
shuleni hapo.
Kibusu amekarabati vyumba hivyo kwa kufumua sakafu iliyokuwa imechimbika na kuchapia kuta zote nje na ndani na bado anaendelea kufanya kazi hiyo.
Kibusu ambaye ni miongoni mwa wachimbaji wadogo wa madini ya Dhahabu kijijini hapo, anasema alifikia uamzi huo baada ya kuona vyumba hivyo vina hali mbaya na kwamba vinaweza kusababisha wanafunzi kukata tamaa.
Anasema ukarabati huo wa vyumba pamoja na ofisi, hadi sasa umegharimu Sh milioni sita na kwamba gharama hiyo itaongezeka akishamaliza ukarababi wote.
Anasema fedha hizo ni sehemu ya faida anayopata kutoka kwenye shughuli zake za uchimbaji wa madini ambazo aliamua kuwasaidia watoto wa eneo hilo.
Anasema hakuna taifa ambalo linaweza kuendelea bila kuwekeza katika sekta ya elimu, hivyo ndio maana kaamua kuwekeza shuleni hapo.
Anasema katika Kijiji cha Itumbi, kumekuwapo wachimbaji wengi wa madini ya dhahabu ambao wamekuwa wakijipatia mamilioni ya fedha lakini wameshindwa kuwasaidia watoto ambao ni taifa la leo.
“Si kwamba mimi nina fedha nyingi kiasi cha kuweza kuwashinda wachimbaji
wenzangu la hasha! Ninachofanya ni kujitolea kuwasaidia watoto wetu katika kukarabati majengo wanayopatia elimu,” anasema Kibusu na kuongeza:
wenzangu la hasha! Ninachofanya ni kujitolea kuwasaidia watoto wetu katika kukarabati majengo wanayopatia elimu,” anasema Kibusu na kuongeza:
“Kuna wachimbaji wengi mno wa Dhahabu wilayani hapa, kwa sababu hii ilitakiwa watoto wetu wasipate shida ya kusoma katika miundombinu mibovu, ikiwa ni pamoja na huduma zingine kama afya, iliapaswa kuwekeze fedha zetu katika hilo.”
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Apolinary Michael anasema shule hiyo ilijengwa mwaka 2000 na ina jumla ya wanafunzi 667 huku ikiwa na vyumba vya madarasa sita ambavyo licha ya uchache wake vilikuwa vimechakaa.
Anasema wanafunzi kuanzia darasa la kwanza hadi la saba ni 482 huku wanafunzi wa shule ya awali wakiwa ni 182 hivyo kufanya idadi ya wanafunzi hao kufikia 667.
Anaeleza kuwa walimu waliopo ni sita huku kukiwa na uhitaji wa walimu tisa, hivyo kwa wastani ni kwamba mwalimu moja anafundisha wanafunzi zaidi ya 100 ikiwa ni tofauti na inavyotakiwa.
Michael anasema vyumba hivyo tangu vimeanza kutumika vilikuwa havijawahi kufanyiwa ukarabati wa aina yoyote mpaka pale Kibusu alipojitolea kuanza kufanya ukarabati mwaka jana.
Anasema kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo shuleni hapo, vinahitajika vyumba 15 na hivyo shule ina upungufu wa vyumba tisa.
“Tunaomba Watanzania wengine kujitolea kujenga miundombinu ya shule,” anaomba msaada mwalimu huyo.
Mwalimu Michael anakiri kuwa upungufu wa vyumba hivyo uliongezeka zaidi baada ya sera ya elimu bila malipo kuanza ambapo watoto wengi waliandikishwa na kusababisha vyumba hivyo kutotosheleza idadi ya wanafunzi.
Anasema katika kila chumba wanakaa wanafunzi zaidi ya 100 huku wale wa darasa la awali wakiwekewa turubai nje ya madarasa kwa ajili ya kuwafundishia kama darasa.
“Hata mimi nilipohamishiwa katika shule hii nilishangaa kuona miundombinu si rafiki kwa watoto kutokana na kuchakaa na nilipojaribu kuitisha mkutano wa wazazi kuweza kujangia suala hili kulikuwapo na kutoelewana,” anasema Mwalimu Michael.
Mwalimu huyo anaeleza changamoto nyingine kuwa ni uchache wa nyumba za walimu ambapo wanalazimika kukaa nyumba moja familia ya walimu watatu ikiwa ni kinyume na utaratibu unavyotakiwa.
Mwalimu mwingine Edwin Mwasoya anasema kuna changamoto kubwa ya wanafunzi kurundikana kwenye darasa moja hivyo kufanya shughuli hiyo ya ufundishaji kuwa ngumu.
Anasema kawaida darasa moja linatakiwa kuwa na wanafunzi 45 hivyo kitendo cha wanafunzi kurundikana kwenye darasa moja kinawafanya walimu washindwe kufahamu nani ameelewa na nani hajaelewa pindi wanapofundisha.
Mwasoya anaeleza kuwa wachimbaji katika kijiji hicho wanatakiwa kujitolea kuweza kujenga miundombinu ya shule hasa madarasa ambayo yamekuwa ni kero kubwa na kuwanyima raha walimu wanapofundisha.
Akizungumza kwenye mkutano wa Hadhara uliofanyika katika kijiji hicho, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Rehema Madusa alimpongeza Kibusu kwa moyo wa kujitolea aliouonyesha kwenye shule hiyo.
Anasema wachimbaji wengine wilayani humo wanatakiwa waige mfano wa mchimbaji huyo kwa kujitoa katika shughuli za kijamii ili ziweze kuimarika katika maeneo yao na si kuisubiri Serikali pekee.
Madusa anasema baadhi ya wananchi wa vijiji vyenye madini wilayani humo hawajishughulishi na shughuli za uchimbaji hivyo wachimbaji wakiboresha huduma hizo, itakuwa ni fursa ya kuwasaidia wananchi hao kunufaika pia na rasilimali hiyo.
“Kuna wananchi ambao hawajishughulishi na uchimbaji wa haya madini hivyo waliojaaliwa kufanya shughuli hii inatakiwa nao wachangie huduma mbalimbali kwa jamii na hao wasiochimba waweze kunufaika kupitia hizo huduma,” anasema Madusa.
Anasema mchimbaji huyo aliamua kutoa kipato ambacho anakipata kupitia uchimbaji wa Dhahabu katika kijiji hicho na kuona ni vyema aweze kuwasaidia watoto wanaopata elimu katika miundombinu mibaya na wakati wana rasilimali ya madini.
Anasema wachimbaji ambao wamekuwa wakifanya shughuli hiyo wanatakiwa kuwekeza zaidi katika elimu ili kuweza kuhakikisha watoto wananufaika na madini hayo kwa kupitia elimu.
Madusa anasema katika wilaya hiyo asilimia kubwa ya ardhi yake ni madini, lakini kumekuwapo na miundombinu mibaya ya elimu hususani madarsa na nyumba za walimu ambao wamekuwa wakipata shida ya kulazimika kupanga mitaani.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wanasema kuna watu ambao wamekuwa wakifanya shughuli zao katika kijiji cha Itumbi na kukusanya marudio ya dhahabu na kuuza zaidi ya milioni 80 lakini wanaona kuwekeza katika elimu kwa kuwatengenezea miundombinu iliyobora wanafunzi ni kosa kwao.
John Ngwandu mkazi wa kijiji cha Itumbi anasema wachimbaji wakiwa na umoja wa kuweza kujitoa katika kuchangia shughuli za kijamii, kijiji hicho kitakuwa na maendeleo.
Anasema katika kijiji hicho kumekuwapo na watu wengi ambao ni wachimbaji lakini hakuna huduma za kiafya hali ambayo imekuwa ni changamoto kwa wananchi wanaoishi eneo hilo.
“Wananchi wanatembea umbali wa zaidi ya kilomita 11 wakifuata huduma afya lakini kuna wachimbaji wengi ambao wakichangishana na kujitoa kwa moyo wote wanaweza kujenga zahanati hata kituo cha afya na wananchi wakaacha kupata shida,” anafafanua Ngwandu.
Ngwandu anasema wachimbaji wanatakiwa kuwekeza kwenye afya na elimu zaidi kwani hawa watoto ni taifa letu na wanahitaji kupata elimu ambayo itakuwa ni mkombozi kwa vizazi vijavyo, pia hata hivyo inakuwa ni njia moja wapo ya kuweza kurudisha fadhila kwa wananchi,” anasema Ngwandu.
Mwananchi huyo anasema sambamba na kujenga miundombinu ya shule hiyo, mchimbaji huyo ameweza kuajili vijana 36 ambao wanaweza kushughulika katika kuhakikisha wanajipatia kipato chao cha kawaida.
Anaeleza kuwa hata vijana wake wamekuwa na mwamko mkubwa wa kuchangia shughuli za kielimu kwa kutoa michango ya ujenzi wa shule hiyo ya msingi.
Ambele Mwakage mkazi wa kijijini hapo, anasema hapo kuna kampuni kubwa ya uchimbaji wa madini Dhahabu lakini kumekuwapo na ugumu wa uchangiaji wa huduma za kijamii.
Anaeleza kuwa kama watu wengi wangekuwa kama Kibusu, kijiji hicho kisingekuwa na shida hata ya kutumia maji yenye kemikali zinazotumiwa na
wachimbaji wakati wa kusafisha madini hayo.
wachimbaji wakati wa kusafisha madini hayo.
Sign up here with your email