MASWALI TATA , MAJIBU TATA , YA PROFESA LIPUMBA - Rhevan Media

MASWALI TATA , MAJIBU TATA , YA PROFESA LIPUMBA

Mwenyekiti wa CUF anayetambulika na Ofisi ya
Mwenyekiti wa CUF anayetambulika na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Profesa Ibrahim Lipumba (kulia) akizungumza alipokuwa akifanyiwa mahojiano na watangazaji wa kipindi cha 360 cha Clouds TV, Baby Kabae (kushoto) na Hassan Ngoma jijini Dar es Salaam jana. Na Mpiga Maalumu 

Dar es Salaam. Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye ana mgogoro na chama chake cha CUF, jana alitinga studio za Clouds TV kujibu mapigo ya hasimu wake, Maalim Seif Sharif Hamad katika kipindi cha 360 na mambo matatu yalijitokeza.
Alichukua hatua hiyo baada ya kipindi hicho cha 360 kumuhoji Maalim Seif juzi na kumsukumia lawama Profesa Lipumba kuwa ndiye anayesababisha mgogoro katika chama hicho, akisaidiwa na Serikali.
Maalim Seif, ambaye alimtuhumu Lipumba kuwa msaliti, alisema ni bora kukaa meza moja na CCM kuliko mwanasiasa huyo msomi wa uchumi kwa kuwa chama hicho tawala kinajulikana kuwa adui wa CUF hivyo ni rahisi kuchukua tahadhari.
CUF ipo katika mgogoro baada ya Profesa Lipumba kuandika barua ya kujiuzulu wadhifa wake Agosti 2015 kwa kile alichoeleza kuwa nafsi inamsuta na mwaka mmoja baadaye aliandika barua ya kubatilisha uamuzi huo.
Hata hivyo Mkutano Mkuu wa CUF, uliofanyika Hotel ya Blue Pearl jijini Dar es Salaam, haukukubali Profesa Lipumba kurejea madarakani, badala yake ukakubaliana na barua yake ya kujivua nyadhifa zote, hali iliyoanzisha mgogoro na viongozi wenzake.
Katika mahojiano hayo ya jana, Profesa Lipumba alizungumza na kujibu mambo mbalimbali lakini kati ya hayo, masuala matatu yalikuwa na utata zaidi.
Jambo la kwanza ni pale Profesa Lipumba alipoulizwa na watangazaji wa kipindi hicho sababu za kwenda kuhudhuria Mkutano Mkuu wa CUF uliofanyika Agosti 21, 2016 wakati hakuwa mjumbe.
Lipumba alijibu kuwa aliitwa na baadhi ya wajumbe wa mkutano huo ambao alisema walimtumia ujumbe mfupi wa simu na baadhi kumpigia simu.
“Nilipigiwa simu na wajumbe 12 wakiniambia ‘hapa kwenye mkutano mkuu, barua yako (ya kujiuzulu) inasomwa. Sisi wajumbe tunataka uje uthibitishe hii barua ndiyo yenyewe uliyoandika?” alisema Lipumba.
“Nilipata simu kama kumi au kumi na mbili. Nikaamua kwenda kwenye eneo la Mkutano Mkuu.Niliondoka nyumbani mimi na dereva mpaka kwenye Mkutano Mkuu.”
Maelezo hayo yalimfanya mtangazaji aulize sababu za kwenda kwenye Mkutano Mkuu wakati hajaalikwa na si mjumbe wa mkutano huo.
“Ah! Mimi nimeitwa na wajumbe kwamba hapa unahitajika kuja kuthibitisha,” alisema na kupandishiwa swali jingine.
“Hiyo imekaaje kikanuni. Unapotakiwa kuja kuthibitisha, kikanuni imekaaje. Unaalikwa kwa kutumiwa barua?” aliulizwa.
“Hapana nilitumiwa ujumbe wa simu. Katika taratibu zetu sisi ujumbe wa simu, barua ni utaratibu halali kumualika mtu kuhudhuria kikao,” alisema.
“Sasa sikujua nani ana-chair (mwenyekiti) nani katibu wa kikao kile, lakini nimekwenda kwenye mkutano mkuu. Nimefika eneo la mkutano nimekuta vijana, walinzi wa chama, blue guard, Nimeshuka wamenipokea, wakaniingiza ndani ya ukumbi wa Mkutano Mkuu. Wakanipeleka mahali nikaenda kukaa.”
Alisema alikuta mjadala kuhusu aitwe kujieleza, lakini mwenyekiti (Julius Mtatiro) alikataa na baada ya mapumziko, walipiga kura na kutangaza matokeo kuwa waliokuwa wanamtaka Lipumba ni wajumbe 14 na waliomkataa ni 476.
“Hiki ndicho chanzo cha sokomoko kutokea na kusababisha wajumbe kuimba ‘ni heri ya Jecha (Salim Jecha) aliyefuta matokeo kuliko Maalim Seif kutangaza matokeo wakati kura hazikupigwa’,” alisema Profesa Lipumba.
Jecha ni mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Mahojiano hayo pia yalijikita katika sababu za uamuzi wa Lipumba kujiuzulu.
Katika mahojiano hayo, Lipumba alisema aliamua kujiuzulu kwa sababu aliona si sahihi kwa Edward Lowassa kuingia ndani ya Ukawa na kugombea urais na kwamba hakuwa kinara wa kumshawishi Lowassa kujiunga upinzani.
“Ni uongo na mimi nilipata taarifa kutoka kwa (mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James) Mbatia kuwa Lowassa anahitaji kuzungumza na mimi na hata siku moja sikuwahi kuomba niunganishwe naye,” alisema.
Aliongeza kuwa hata siku moja hakuwahi kuomba namba ya Lowassa.
Alipotafutwa jana, Mbatia alisema hawezi kuzungumza chochote kwa sasa kuhusu kinachoendelea ndani ya CUF.
Juzi, Maalim Seif alisema ana ushahidi kuwa Profesa Lipumba alikwenda kumtafuta Lowassa ajiunge na Ukawa na alimuomba Mbatia amuunganishe naye.
Wakati akimkaribisha Lowassa ndani ya Ukawa Julai 2015, Profesa Lipumba alisema suala la ufisadi ni mfumo na si la mtu mmoja mmoja.
“Sisi tunaponda ufisadi na mfumo wa kifisadi na chanzo kikubwa cha ufisadi ni mfumo ndani ya CCM, kwanza tuing’oe CCM, hapo ndipo tutakapoweza kuondoa ufisadi,” alisema Lipumba wakati wa kumtambulisha Lowassa wakati huo.
“Lowassa alikumbwa na tuhuma za ufisadi mwaka 2008, leo ni 2015 lakini ufisadi umeongezeka au umepungua? Lowassa hayupo serikalini? Tatizo ni mfumo na jambo la kwanza ni kuing’oa CCM.”
Lakini jana, Lipumba alisema kuwa hakusema Lowassa ndiye awe kamanda wa kuongoza vita dhidi ya ufisadi.
Hata hivyo, katika mahojiano hayo Profesa Lipumba alikiri kwenda nyumbani kwa Lowassa na kufanya mazungumzo kuhusu watu wanaomuunga mkono kujiunga na Ukawa.
Alieleza kuwa mipango yote ilisukwa na Chadema na kitendo cha yeye kuhusishwa katika mchakato wa kumshawishi Lowassa ulikuwa ni propaganda.
Alisema hatua yake ya kumlaumu Maalim Seif imetokana na katibu huyo mkuu huyo kufanya vikao na Chadema bila kumshirikisha yeye.
Kuhusu nguvu yake ndani ya CUF, Profesa Lipumba alisema baadhi ya wanachama walimfuata kumshawishi ashiriki kampeni kwa kuwa walimtambua kama bado mwenyekiti.
“Walikuja kina mbunge wa Temeke, Abdallah) Mtolea na (mbunge wa Kinondoni, Maulid) Mtulia kuniomba nishiriki kampeni zao, nikawaeleza siwezi kutokana na hali ilivyo kwa kuwa nitaharibu uhusiano kati yao na Chadema,” alisema
Akizungumzia suala hilo jana, Mtolea alithibitisha kuwa alienda kwa Lipumba kumuomba ahudhurie uzinduzi wa kampeni kama mwanachama wa kawaida.
“Nilimuomba akanikatila kwa sababu ya Lowassa. Nikamweleza mkutano ni wangu mimi siyo wa Lowassa akakataa pia,” alisema Mtolea.
Kuhusu kuwa msaliti, Lipumba alisema “waliosaliti ni wale waliofanya utaratibu wa kumleta Lowassa”.
Sababu za kujiuzulu,
Akizungumzia sababu za kujizulu, Profesa Lipumba alisema ni ukosefu wa umoja ndani ya CUF, hasa baada ya Ukawa kuundwa.
Alisema wakati mwingine, vikao vilifanyika bila yeye kupewa taarifa. “Nikajikuta nina wakati mgumu kulinda maslahi ya umoja na maslahi ya chama na ukosefu huu ulitumiwa na Chadema kuwadhalilisha wagombea wa CUF Bara,” alisema.
Alisema Chadema walisema CUF haina fedha za kusimamisha mgombea na taarifa hizo walipewa na Maalim Seif.
Kuingia ofisini
Profesa Lipumba alisema baada ya Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa kumtambua kama Mwenyekiti alikwenda moja kwa moja hadi ofisi ya makao ya chama hicho, Buguruni na kukanusha kuwa hakuvamia.
Alisema anamtambua Maalim Seif kama Katibu Mkuu, lakini alishangaa kwa nini hafiki ofisini.
Alisema tayari ameshamwandikia barua ya kuitisha kikao cha kamati tendaji kisha Baraza Kuu la Uongozi.
Aliongeza kuwa hakuanza kutofautiana na Maalim Seif baada ya kujiuzulu bali wakati wa mchakato wa maoni ya Rasimu ya Katiba mpya.
Alisema Maalim Seif alitaka muungano wa mkataba wakati msimamo wa chama ilikuwa ni Serikali tatu.
CUF ina wabunge 42, na kati ya hao ni wawili tu wanaomuunga mkono Profesa Lipumba.     







Previous
Next Post »