BAJETI YA WIZARA YA AFYA YAIBUA ' VILIO' - Rhevan Media

BAJETI YA WIZARA YA AFYA YAIBUA ' VILIO'

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2017/18, mjini Dodoma. Picha na Anthony Siame      

Dar es Salaam. Bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ilihitimishwa bungeni jana kwa ‘vilio’ kutoka kwa wabunge juu ya matatizo ya uhaba wa dawa, huduma duni za afya na kukithiri kwa matukio ya ubakaji na ulawiti.
Hawakuishia hapo, walielezea ukubwa wa changamoto nyingine ya magonjwa na vifo vya wajawazito wakiitaka Serikali kuyavalia njuga huku wakifufua hoja ya kikombe cha Babu wa Loliondo.
Wakichangia hotuba hiyo iliyowasilishwa juzi na waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu, wabunge hao pia waliibua masuala ya upungufu wa madaktari na watendaji wengine wa afya, upungufu wa vifaa vya tiba na madeni ya madaktari.
Ummy aliliomba Bunge kuidhinishiwa Sh 1.1 trilioni katika bajeti ya mwaka 2017/18. Katika bajeti ya mwaka jana, wizara hiyo iliidhinishiwa Sh796.1 bilioni lakini zilizotolewa na Serikali ni asilimia 40 tu.
Katika mchango wake, Mbunge wa Vunjo, James Mbatia alisema jinsi Watanzania wengi wakiwamo viongozi wa Serikali walivyokimbilia kwa Babu wa Loliondo ni ishara kuwa wengi wanaumwa na kuna tatizo kubwa katika sekta ya Afya.
“Watu wangapi walikwenda Loliondo kupata kikombe cha Babu, wangapi walifia huko na hata Serikali nzima ikahamia huko,” alihoji Mbatia.
Mbatia alikuwa anakumbushia jinsi maelefu ya Watanzania na wengine wa nchi jirani walivyomiminika kwa Mchungaji Ambilikile Masapila katika Kijiji cha Samunge, Liliondo kunywa kikombe cha dawa aliyodai ameoteshwa kutibu magonjwa yote sugu.
Mbunge huyo alisema kutokana na huduma mbovu, hali ya afya nchini inatisha na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinasema ifikapo mwaka 2030, Watanzania 42,000 watakufa kwa saratani na 68,000 watakufa kwa magonjwa ya ajali.
Aliwataka wabunge kuacha itikadi zao na kutumia mamlaka yao kikatiba kuitaka Serikali kuongeza fedha za afya.
Mbunge wa Kinondoni (CUF), Maulidi Mtulia alisema Hospitali ya Mwananyamala haipati ruzuku ya Serikali hivyo kuipa mzigo Halmashauri ya Kinondoni.
Mbunge huyo alitumia ilani ya CCM kujenga hoja yake kuwa chama hicho kiliahidi kujenga kituo cha afya kila kata na wananchi wakaichagua, hivyo kuitaka itekeleze la sivyo atawaeleza wananchi kuwa iliwalaghai.
Mjadala huo uliibua pia madhara ya tetemeko la Septemba mwaka jana mkoani Kagera pale Mbunge wa Bokoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare aliposema zahanati nne na vituo vya afya viwili vilivyobomoka kabisa na havijajengwa hadi leo licha ya kamati ya maafa kuvitengea Sh380 milioni.
Mbunge wa Morogoro Mjini (CCM), Abdulaziz Abood, aliomba Serikali kupunguza gharama za matibabu kwa wagonjwa wanaovunjika mifupa kwenye ajali.
Alisema wamekuwa wakilipa Sh500,000 na sasa ni Sh700,000 kwa kila anayevunjika.
“Wanapouliza kulikoni walipie gharama hizo, wanaambiwa ni kwa sababu ya vyuma lakini wengine hawana uwezo kiuchumi. Tusaidie tupate vifaa hivi ili kupunguza gharama,” alisema.
Hussein Bashe (Nzega Mjini-CCM) alilalamikia mashine ya X-Ray iliyoharibika katika Hospitali ya Wilaya Nzega kutotengenezwa kwa miezi mitano tangu Januari.
Alisema kampuni inayotengeneza mashine hizo ya Philips ilipewa kazi hiyo, lakini ilichelewa. “Aliambiwa aje afanye Service ya X-Ray, lakini kila akipigiwa simu anasema anakuja lakini haji. Lakini mkurugenzi wa halmashauri aliamua kuchukua mtaalamu katika Hospitali ya Bugando ambaye alikuja na kuchukua kifaa kwenda kutengeneza,” alisema huku akimwomba Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene asimchukulie hatua kwa uamuzi huo.
Pia wabunge wa Viti Maalumu–CCM, Faida Bakari na Amina Mollel walijadili kwa uchungu suala la unyanyasaji wa watoto na ubakaji.
Bakari alimwaga machozi wakati akichangia suala hilo huku Mollel akiibua kashfa nzito ya nchi za Magharibi kutoa fedha kwa walimu wa madarasa na shule za msingi ili kulawiti watoto na kutengeneza mashoga.
Mbunge huyo alisema anayo ripoti ya utafiti huo na ilishakabidhiwa kwa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
Maoni ya Wadau
Akizungumzia bajeti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Sikika, Irenei Kiria alisema ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa dawa, ni muhimu kwa Serikali kuiruhusu sekta binafsi kutoa huduma za afya ikiwamo kununua na kuzalisha dawa nchini.
Alisema huduma nyingi za afya zipo chini ya Serikali huku bajeti yake ikiwa finyu hali inayosababisha ukosefu wa ajira za madaktari pamoja na upungufu wa vifaa vya tiba.
Alisema takwimu za Serikali zinaonyesha kuwa hadi sasa kuna madaktari 2,790 tu ambao hawakidhi mahitaji.
Kwa makadirio ya idadi ya watu 50 milioni waliopo Tanzania, ili kufikia viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO) inatakiwa kuwa na madaktari 6,250. “Hii ina maana kuwa Tanzania ina upungufu wa madaktari 3,640 sawa na asilimia 55.4 katika hospitali zake,” alisema Kiria.
Hivi karibuni Serikali ilitangaza kuwaajiri madaktari 500 waliojitokeza kwenda kufanya kazi Kenya baada ya nchi hiyo kuiomba Tanzania kabla ya mpango huo kuvurugika.
Kuhusu ukatili dhidi ya watoto, Mkurugenzi wa Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo Bi-Simba alisema ongezeko la matukio hayo linatokana na ukosefu wa uangalizi kwa watoto nyumbani na wakati wanapokwenda shuleni. Ripoti ya kituo hicho ya mwaka 2016, iliyotolewa juzi na imebainisha kuwa kwa kuanzia Januari hadi Julai 2016, matukio ya ukatili kwa watoto yalikuwa 2,571.
Bi-Simba aliongeza kuwa imani za kishirikina na ukosefu wa maadili baina ya wanajamii imekuwa kichocheo kikubwa cha uhalifu huo.
Akizungumzia vifo vinavyotokana na uzazi, Mwenyekiti wa Shirika la Afya na Elimu ya Tiba (Tahmef), Juliana Busasi alisema kuwa tatizo kubwa ni kutokuwapo ufuatiliaji wa karibu wa maendeleo ya afya wakati wa ujauzito kwa baadhi ya wanawake.
Alisema pia upungufu wa vifaa katika vituo vya afya unasababisha wazazi kupoteza maisha wakati wa kujifungua na kuwataka wadau na Serikali kuwekeza katika kununua vifaa vya kutosha.
“Changamoto nyingi zinazojitokeza wakati wa uzazi zinatokana na vichochezi wakati wa ujauzito. Zinapotokea na kama hospitali hakuna vifaa mgonjwa anaweza kukosa msaada,” alisema.
Katika bajeti yake, Waziri Mwalimu alisema Sh1.8 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kuendeleza huduma za uzazi za dharura.
Kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, daktari kutoka Chama cha Afya ya Jamii Tanzania, Ali Mzige alisema Wizara ya Afya haina budi kujikita katika kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa kutoa elimu.
Alisema matangazo ya elimu kuhusu mfumo wa maisha yanaweza kusaidia kuimarisha afya bora ingawa sasa wengi wanatangaza biashara.     







Previous
Next Post »