Mkazi wa kijiji cha Ikungi wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida, Herman Joseph (32), amefariki dunia papo hapo baada ya kupigwa risasi tumboni na kutokea upande wa pili na askari Polisi aliyekuwa akijihami.
Kwa mujibu wa ofisi ya Kamanda Polisi mkoa kwa sasa si salama kutajwa jina la Polisi aliyesababisha kifo hicho.
Tukio hilo limetokea Machi, 14 mwaka huu saa 9.45 alasiri huko maeneo ya Ikungi madukani makao makuu ya wilaya ya Ikungi.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, ACP Debora Magiligimba, alisema kuwa siku ya tukio Herman alimfuata mke wake ambaye ni mama lishe katika vibanda vilivyoko kando kando na barabara kuu ya Singida-Dodoma.
Alisema Herman alipofika kibandani alimwomba mke wake Maria Jacob (28) amwandalie chakula cha mchana. Hata hivyo kulizuka malumbano yaliyopelekea mume (Herman) kuchomoa kisu kutoka kwenye mfuko wa suruali.
“Alipoona kisu, Maria alianza kuokoa maisha yake kwa kukimbia huku akiwa amebeba mtoto mgongoni. Wakati akiendelea kukimbia, Herman alifanikiwa kumchoma kisu mke wake sehemu ya makalio,” alisema.
Alisema kuwa baada ya kuchomwa kisu, Maria alikimbilia kujificha kwenye kibanda cha Janeth Mathias (28).
“Baada ya kupiga yowe, Shaban Jumanne (35) na Issa Shaban (48) walifika eneo la tukio. Shaban alijeruhiwa vibaya mkono wa kulia na Issa mkono wa kushoto.Baada ya hapo taarifa iliweza kufika katika kituo kidogo cha Polisi Ikungi. Haraka askari wanne wakiwa na bunduki, walifika eneo la tukio,” alisema.
Alisema askari Polisi hao waliokuwa wakiongozwa na DC H 8794, Mavura, walikuta Herman tayari amejificha ndani ya kibanda. Hakuchukua muda alitoka nje ya kibanda, na kutangaza haogopi chochote na yupo tayari kuuawa.
“Baada ya kutakiwa kujisalimisha, hakutii badala yake alimfuata askari aliyekuwa na silaha na kutaka kumchoma kisu kifuani, askari alikikwepa. Askari huyo aliweza kupiga risasi mbili hewani kwa lengo la kumwogofya,” alisema.
Hata hivyo alisema Herman hakuweza kuogopa aliendelea kumfuata na wakati askari huyo akirudi nyuma, aliteleza na kuanguka chini. Wakati akiwa chini, ndipo Herman alipotaka kumchoma kifuani kwa kisu.Askari aliamua kijihami kwa kumpiga risasi.
Kamanda Magiligimba, alisema kifungu 21 mwenendo wa makosa ya jinai 20 cha mwaka 1985, kinaruhu askari kuua kwa lengo la kulinda maisha yake au ya watu wengine.
Sign up here with your email