SIR KAHAMA ALITEKELEZA AZIMIO LA ARUSHA – MWAPACHU - Rhevan Media

SIR KAHAMA ALITEKELEZA AZIMIO LA ARUSHA – MWAPACHU

Tokeo la picha la AZIMIO LA ARUSHA

WAZIRI mstaafu wa Katiba na Sheria, Bakari Mwapachu, amemzungumzia marehemu Sir George Kahama, kuwa ni miongoni mwa viongozi waliotekeleza Azimio la Arusha mwaka 1967.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwa marehemu Dar es Salaam jana, Mwapachu alisema baada ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere kupitisha azimio hilo, Sir Kahama aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).
Alisema miongoni mwa majukumu aliyokuwa akiyatekeleza, ni pamoja na kusimamia sera ya utaifishaji wa mali za wakoloni, vikiwamo viwanda, mashamba na mashirika ya utalii na kuanzisha viwanda vingine vya uzalishaji mali.
“Baada ya kupitishwa kwa Azimio la Arusha, Sir Kahama aliweza kusimamia vema utaifishwaji wa mali za wakoloni vikiwamo viwanda, mashamba na mashirika ya utalii na kuviweka chini ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC),” alisema Mwapachu.
Alisema licha ya kutaifishwa kwa mali hizo, aliweza kuanzisha Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambavyo vyote vilikuwa chini ya NDC.
Mwapachu alisema kutokana na hali hiyo, aliweza kuanzisha viwanda vipya katika kipindi cha Serikali ya awamu ya kwanza, jambo ambalo lilisaidia taifa kupata maendeleo.
Alisema  katika kipindi chake cha uongozi, aliwahimiza wafanyakazi wake kupata kozi mbalimbali za mafunzo ili kuongeza ujuzi na utendaji kazini, jambo ambalo lilisaidia viongozi wengi kuwa na weledi na uadilifu.
“Nitamkumbuka kwa mengi sana… kwa sababu yeye ndiye aliyetufundisha kazi katika kipindi hicho, tukiwa mimi na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba.
“Kutokana na msimamo wake, aliweza kuhimiza watendaji kusimamia Azimio la Arusha kwa vitendo, jambo ambalo lilisaidia utekelezaji wake kufanyika kwa vitendo,” alisema.
Mbali ya Mwapachu, viongozi mbalimbali walifika nyumbani kwa marehemu kuwafariji wafiwa.
Viongozi hao ni pamoja na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya, aliyekuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Basil Mramba na aliyekuwa Spika wa Bunge la Afrika, Getrude Mongela.
Sir Kahama alifariki juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako alikuwa amelazwa kupatiwa matibabu.
Mwili wa marehemu utaagwa leo katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) kuanzia saa nne asubuhi hadi saa saba mchana.
Kesho mwili utasaliwa katika Kanisa la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay.
Marehemu ameacha mjane na watoto wanane.
Previous
Next Post »