MVUA za masika zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini, zinatarajiwa kuendelea hadi mwezi Mei mwaka huu.
Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani na juu ya wastani katika baadhi ya maeneo nchini huku mingine yakitarajiwa kupata mvua za wastani na chini ya wastani.
Akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake jana, Meneja Mtandao wa Vituo na Msimamizi wa huduma za hali ya hewa kwa Jamii, Hellen Msemo, aliyataja maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani na juu ya wastani kuwa ni pamoja na mikoa yote ya Kanda ya Ziwa.
Maeneo mengine ni Kanda ya Magharibi inayojumuisha mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa, Nyanda za juu Kusini Magharibi mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa na Kaskazini mwa Morogoro, Kusini na Pwani ya Kusini Ruvuma, Lindi na Mtwara.
Aliyataja maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani na chini ya wastani kuwa ni pamoja na Pwani ya Kaskazini Mashariki ambayo ina mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani na visiwa vya Unguja na Pemba, Nyanda za juu Kaskazini Mashariki ni Kilimajaro, Arusha na Manyara.
Alisema maeneo mengi ya nchi tayari yameanza kupata mvua tangu wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Machi, huku baadhi yakitarajiwa kupata mvua muda wowote.
“Kutokana na mifumo ya hali ya hewa iliyopo na inayotarajiwa, kuna uwezekano mkubwa wa mvua za wastani katika maeneo mengi, hata hivyo mtawanyiko hafifu wa mvua na vipindi virefu vya ukavu vinatarajiwa kujitokeza katika kipindi hiki cha mvua za msimu,” alisema Msemo.
Aidha, alisema mikoa ya Singida na Dodoma ambayo kwa kawaida hupata mvua msimu mmoja kwa mwaka, mvua hizo zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Aprili.
Aliwataka wananchi hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua juu ya wastani kuendelea kufuatilia taarifa zinazotolewa na TMA na kuchukua hatua za kiusalama kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na mvua zinazoendelea.
“Miongoni mwa majukumu yetu ni kuhakikisha usalama wa mali za wananchi na uhai wao na taarifa zinaonyesha kutakuwa na vipindi vifupi vya mvua kubwa, hivyo wanapaswa kuendelea kufuatilia taarifa zetu,” alisema Msemo.
Sign up here with your email