Wakati elimu ikitajwa kuwa moja ya haki za msingi kwa kila mtoto, Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa watu wenye ulemavu kilichopo Mjini Singida, kimelazimika kuanza kukataa kuwapokea baadhi ya wanafunzi wenye ualbino kutokana na kuhofia hali tete ya usalama wa maisha yao.
Imeelezwa kuwa kutokana na vitendo vya ukataji viongo kwa jamii hiyo kwa imani za ushirikina, Chuo hicho kimekataa baadhi ya maombi ya wenye ualbino waliotaka kujiunga na kozi za ufundi, kwa kuwa hakuna uzio wa uhakika na kuna mlinzi mmoja tu asiyeweza kufanyakazi usiku na mchana,
Hayo yalisemwa juzi na Mkuu wa Chuo hicho cha ufundi, Fatuma Malenga wakati akitoa taarifa yake kwa uongozi wa jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT) mkoa wa Singida uliofika chuoni hapo kutoa msaada ukiwemo vyakula na vinywaji.
Mkuu wa Chuo hicho Fatuma Malenga pamoja kushuruku kwa msaada huo alisema zipo changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa uzio wa uhakika na walinzi kiasi cha kulazimika kukataa kuwapokea baadhi ya wanafunzi wenye ualbino kwa kuhofia usalama wao wakiwa shuleni.
Mbunge wa viti maalum (CCM) mkoa wa Singida,Aysharose Mattembe,akimkabidhi mmoja wa wanafunzi wa chuo cha ufundi cha walemavu mjini hapa,Kashinde Athumani,baadhi ya soda zilizotolewa na jumuiya ya wanawake Tanzania mkoa wa Singida kwa wanafunzi wa chuo hicho. Pamoja na soda na maji,pia walipewa mchele kilo 50 na mafuta ya mbonga lita 20. (Picha na Nathaniel Limu)
Alisema kutokana na watu wenye ualibino kusakwa kukatwa viungo vyao na baadhi ya watu wenye imani potofu kuwa vinaweza kuwatajirisha haraka, chuo kimeshindwa kuwapokea kwa madai hakutakuwa na ulinzi wa kuaminika.
“Chuo chetu kinatoa mafunzo kwa walemavu mbalimbali wakiwemo kutoka kwenye ajira ya serikali.Lakini kwa ndugu zetu hawa wenye ualibino,tunawapenda sana, lakini hatuna ulunzi mzuri kwa ajili yao,” alisema Malenga.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika halfa hiyo, Mwenyekiti wa UWT-mkoa wa Singida, Diana Chilolo, alikiri kuwa changamoto bado ni nyingi zinazohitaji msaada na nguvu ya pamoja kutoka kwa wadau mbalimbali.
Kwa hali hiyo, Chilolo alitumia fursa hiyo kuiomba serikali ya CCM na wadau mbalimbali, kukiangalia chuo hicho kwa jicho la huruma.
Naye Katibu wa UWT mkoa wa Singida, Angela Milembe, alisema lengo la ziara hiyo iliyoambatana na kutoa msaada, pia inalenga kuitambulisha CCM ya Jumuiya ya Wanawake Tanzania (CWT), kwa wanafunzi hao walemavu pamoja na walimu wao.
Mwenyekiti wa jumuiya ya wanawake Tanzania mkoa wa Singida, Diana Chilolo,akimkabidhi mkuu wa chuo cha ufundi cha walemavu mjini hapa, Fatuma Malenga msaada uliotolewa na UWT mkoa wa Singida.Msaada huo ni pamoja na soda,maji,mchele kilo 50 na mafuta ya mboga lita 20.
“Hii ni sehemu ya utekelezaji wa ilani yetu ya CCM, kwamba walemavu nao ni Watanzania sawa na wale ambao hawana ulemavu.Misaada hii pamoja na kupunguza makali ya maisha yao, itawafanya watambue kuwa jamii kwa ujumla,inawathamini,” alisema Milembe.
Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa watu wenye ulemavu Singida kilianzishwa mwaka 1977, lengo likiwa kutoa mafunzo ya ufundi ili kuwawezesha walemavu kujitegemea kwa kujiajiri au kuajiriwa.
Sign up here with your email