UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kumjeruhi Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresa Mmbando, inayomkabili Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema)na wenzake umefunga ushahidi.
Jamhuri ikiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Flontina Sumawe, ilifunga ushahidi huo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Upande wa mashtaka ulifanya hivyo baada ya kuwaita mashahidi wanne kutoa ushahidi kuhusu mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao.
Mahakama imeamuru pande zote mbili kuwasilisha majumuisho ya kesi ili kuisaidia kuona kama washtakiwa wana kesi ya kujibu ama la.
Hoja za utetezi zitawasilishwa Machi 21, mwaka huu na upande wa mashtaka utawasilisha Machi 28, mwaka huu na kama kutakuwapo na nyongeza wawasilishe Aprili 5,2017 siku ambayo kesi itatajwa.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni wabunge, Saed Kubenea (Ubungo) Mdee (Kawe), Mwita Waitara (Ukonga) wote kutoka Chadema.
Wengine ni Diwani wa Kata ya Kimanga, Manase Njema (Chadema), mfanyabiashara na kada wa chama hicho, Rafii Juma na Diwani wa Kata ya Saranga Kimara, Ephreim Kinyafu.
Kwa pamoja wanadaiwa kuwa Februari 27,2016 katika Ukumbi wa Karimjee, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam walifanya kosa la kumjeruhi Theresia na kumsababishia majeraha. Washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana.
Mmbando wakati akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo, alieleza jinsi alivyovamiwa, kujeruhiwa na kupokonywa faili lililokuwa na ajenda na mwongozo wa uchaguzi wa Meya na Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam uliopaswa kufanyika Februari 27,2016.
Alidai kuwa siku hiyo ya Februari 27, 2016 alipewa jukumu la kuusimamia uchaguzi huo wa Meya na Naibu Meya ambao ulipaswa kufanyika saa 4 asubuhi katika Ukumbi wa Karimjee.
Sign up here with your email