MAKAMU WA RAIS “MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA NA UFISADI HAYATARUDI NYUMA KAMWE” - Rhevan Media

MAKAMU WA RAIS “MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA NA UFISADI HAYATARUDI NYUMA KAMWE”

Balozi wa Sweden Nchini Katarina Rangnitt ameunga mkono jitihada za serikali ya awamu wa Tano katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi kama hatua ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kijamii kwa viwango vinavyotakiwa kote nchini.
Balozi huyo wa Sweden nchini Katarina Rangnitt amesema hayo 3 March 2017 baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Balozi Katarina Rangnitt amesisitiza kuwa serikali ya Sweden inafurahishwa sana na jitihada hizo za serikali ambazo zinalenga kukomesha vitendo hivyo vya rushwa na mapambano dhidi ya umaskini ili kusaidia wananchi kuishi maisha mazuri kwa kupata huduma bora zikiwemo za afya,maji na elimu kwa ubora unaotakiwa.
Balozi huyo amesema kuwa Sweden itaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania kwa kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo Tanzania Bara na Zanzibar kama hatua ya kujenga na kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo.
Kuhusu mabadiliko ya tabia ya nchi na masuala ya usawa wa kijinsia, Balozi huyo amesema kuwa nchi yake ipo mstari wa mbele kuhakikisha jitihada za utunzaji wa mazingira zinaimarishwa hivyo serikali ya Sweden ipo tayari kushirikiana kikamilifu na Tanzania katika kukabiliana tatizo hilo.
Kwa upande wake, Makamu  wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan imeipongeza na kuishukuru nchi ya Sweden kwa ufadhili wake katika bajeti ya kuu serikali na kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo hasa kwenye sekta za nishati,elimu, tafiti na afya.
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan amemhakikishia balozi huyo wa Sweden nchini kuwa serikali ya awamu ya Tano itaendelea kupambana ipasavyo na vitendo vya rushwa, kuondoa ukiritimba katika sekta mbalimbali nchini hatua ambazo zitasaidia serikali kupata wawekezaji wengi kutoka mataifa mbalimbali Duniani kuja kuwekeza hapa nchini.

Previous
Next Post »