Je nani anawajibu wa kumtunza mwenzake kati ya wanandoa. Je ni mme, je ni mke au ni wote . Sheria inasemaje kuhusu hili. Kwa kuanza tu ni kuwa suala matunzo kwa wanandoa ni la kisheria. Matunzo sio hisani,zawadi au upendeleo maalum bali ni wajibu uliozaliwa na sheria.
Sheria ya Ndoa iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 , sura ya 29 imeweka bayana habari nzima ya matunzo baina ya wanandoa. Niseme mapema tu kuwa wapo wanaojua kuwa mme peke yake ndiye mwenye wajibu wa kutoa matunzo kwa mke. Tutaona hili likoje .
Kabla ya hayo ni vema tukaona matunzo yanajumuisha nini na nini kwa mujibu wa sheria hii.
1.MATUNZO NI YAPI.
Kifungu cha 63( a ) cha sheria ya ndoa kinataja vitu ambavyo kisheria ndivyo vitakavyoitwa matunzo kwa mwanandoa. Kifungu kinataja makazi(accommodation), mavazi, na chakula. Haya ndiyo ya msingi ambayo mwenye wajibu wa kuyatoa atatakiwa kutoa.
2. MKE KUTOA MATUNZO KWA MME.
Ni vema kujua kuwa suala la matunzo linawahusu wanandoa wote yaani mke pamoja na mme. Kila mmoja anao wajibu kwa mwenzake katika kutoa matunzo. Isipokuwa wajibu huu umetofautiana kati ya hawa wawili . Mke ana wajibu wenye mipaka katika kutoa matunzo halikadhalika mme.
Kifungu cha 63( b ) cha sheria ya ndoa kinasema kuwa mwanamke ambaye ana uwezo anawajibu wa kutoa matunzo kwa mme wake ambaye hajiwezi, ambaye ana ugonjwa wa kimwili au kiakili ambao haumuwezeshi kufanya kazi ya kumuingizia kipato.
Kifungu kiko wazi kuwa wajibu wa mwanamke kumhudumia mwanaume ni pale tu mwanaume huyo anapokuwa mlemavu au mgonjwa wa akili au mwili. Lakini pia ugonjwa huo au ulemavu huo uwe ni wa kiwango cha kutomwezesha kufanya kazi. Ikiwa ugonjwa au ulemavu ni wa kiwango cha kumwezesha kufanya kazi atakuwa nje ya muktadha wa kifungu hiki.
Sign up here with your email