Wananchi wa Wilaya za Rungwe na Mbeya Vijijini pamoja na wadau wengine wa mradi
wa jotoardhi wa Ngozi wametoa maoni mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuuliza maswali ya
msingi kabla ya zoezi la uchorongaji visima vya uchunguzi na baadae uvunaji mvuke wa
kuzalisha umeme utakaotokana na nishati ya jotoardhi.
Wananchi walipata fursa ya kutoa maoni yao kati ya tarehe 6 hadi 11 Machi, 2017, wakati
timu ya wataalamu wa Mazingira na Jamii kutoka Kampuni ya kuendeleza Jotoardhi
Tanzania (TGDC) na TANESCO walipotembelea eneo la mradi, ikiwa ni matakwa ya
kisheria ya kushirikisha wadau na jamii itakayopitiwa na mradi husika, wakati wa kufanya
tathmini ya athari za mradi katika mazingira na jamii.
Maoni yao ilikuwa ni pamoja na kuiomba Serikali kusimamia taratibu za ajira wakati wa
zoezi la uchorongaji visima vya jotoardhi, akizungumza Ndugu Yohana Julius wa Kata ya
Swaya Vijijini alisema “wanaomba ajira zisizohitaji ujuzi wapatiwe wakazi wa eneo la
mradi ili wanufaike moja kwa moja kwa kujiongezea kipato”
Bibi Mary Gwamaka alisema “wanaomba mradi huu usiwaache nyuma wakina mama,
kwani wanao uwezo wa kufanya kazi mbalimbali, hivyo wanaomba wasibaguliwe”
Akijibu moja ya maswali ya wananchi, Mhandisi wa Mazingira kutoka TANESCO Bw.
Fikirini Mtandika alisema sheria na taratibu zote za mazingira zitazingatiwa wakati wote
wa utekelezaji wa mradi chini ya usimamizi wa Baraza la Udhibiti na Usimamizi wa
Mazingira (NEMC) pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira.
“TGDC inaandaa mikakati mbalimbali ya kupunguza na kuziondoa kabisa baadhi ya
athari za mradi huu katika mazingira yetu” aliongezea Mhandisi Mtandika.
Wananchi wa maeneo yote yanayozunguka mradi wa jotoardhi wa Ngozi wameridhia
hatua ya uchorongaji visima vya uchunguzi na baadae uzalishaji umeme na wako tayari
kutoa ushirikiano. Kata zinazopitiwa na mradi huu ni Ijombe, Swaya-Mbeya vijijini, Swaya
Rungwe na Ndanto.
Wananchi wakitoa maoni kwa wataalamu kutoka
TGDC na TANESCO wakati wa mkutano wa kujadili athari na faida za mradi wa jotoardhi
wa Ngozi kweye mazingira na kwa jamii.
Mtaalamu wa Sosholojia Bi. Vaileth Kimaro akizungumza na vikundi vya
wanawake wakati wa kujibu maswali na kupokea maoni kuhusu athari na faida za mradi
wa jotoardhi wa Ngozi kwa jamii na mazingira.
Mhandisi Leonard Masanja (aliyesimama kushoto) akijibu hoja za wananchi
wa Kata ya Ndanto wakati wa mjadala wa athari na faida za mradi wa jotoardhi wa Ngozi
kwa jamii na mazingira, aliyeshika kipaza sauti ni Afisa Maendelea ya Jamii wa Wilaya ya
Rungwe Bi. Rachel Mbelwa
Sign up here with your email