Mojawapo ya madarasa yaliyokamilika katika shule ya msingi Chang’ombe A Manispaa ya Dodoma. Jumla ya vyumba vya madarasa sita vimejengwa ili kukabiliana na changamoto ya vyumba vya madarasa katika shule hiyo inayotokana na wingi wa wanafunzi, shule hiyo ina zaidi ya wanafunzi 2000
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe.Seleman S.Jafo akizungumza na walimu, wanafunzi na Kamati ya shule ya msingi Chang’ombe A Manispaa ya Dodoma alipofanya ziara kujionea maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ambao umekamilka kwa asilimia mia moja. Kulia kwake ni Kaimu Afisa Elimu Mkoa Dodoma Bw. Tumsifu Mwasamale na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bi. Nelly kinyaga kushoto kwake ni Diwani Kata ya Chang’ombe Mhe.Bakari Samweli Fundikira
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe.Seleman S.Jafo akifungua mlango ili kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa ambao umekamilika kwa asilimia mia moja
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe.Seleman S. Jafo akitoa agizo kwa halmashauri, kamati za shule na mikoa nchini kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake kutumia juhudi na maarifa ili kuwaletea wananchi maendeleo kwa haraka. Ameridhishwa na ubora na kasi waliyoitumia kujenga majengo hayo
………………………………………………………………………………………….
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Seleman Jafo amewataka wanafunzi na walimu wa shule ya msingi ya Chang’ombe kutunza na kuitumia miundombinu iliyojengwa ili kuongeza ufaulu katika shule hiyo.
Jafo ametoa kauli hiyo leo alipotembelea shule hiyo ili kukagua utekelezaji wa agizo alilolitoa juu ya kukamilisha ukarabati wa miundombinu katika shule hiyo ifikapo 10 januari, mwaka huu.
Novemba 3, mwaka jana Jafo alitoa agizo kwa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa matundu 20 ya vyoo na vyumba vya madarasa 8 pamoja na ukarabati wa vyumba vya madarasa 2 katika shule ya Chan’gombe A ifikapo januari, 10 mwaka huu kabla ya msimu wa masomo kuanza.
Katika ziara hiyo, Jafo amesema ameridhishwa kwa hatua nzuri ya ukarabati huo na kupongeza uongozi wa Halmashauri ya Manispaa , kamati ya shule ya Chang’ombe ,walimu na Diwani wa Kata ya Chang’ombe kwa utekelezaji huo.
Amesema shule hiyo inapaswa kuongeza ufaulu wake ili iwe mfano mzuri wa kuigwa kwa shule nyingine .
Amesema awali alitoa agizo hilo baada ya kubaini changamoto mbalimbali katika shule ya msingi ya Chang’ombe A .
‘’Maagizo niliyoyatoa yalikuwa magumu sana lakini nia yangu ilikuwa kuwatengenezea mazingira rafiki wanafunzi na walimu , nimefarijika na utekelezaji wake, hali haikua nzuri hapo mwanzo lakini nimefarijika kwa kazi nzuri, muonekano wa madarasa unaridhisha nawapongeza sana’’ amesema Naibu Waziri huyo
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Nelly Kinyaga ameishukuru serikali kwa kuboresha miundombinu ya shule hiyo ambapo awali mazingira ya shule hiyo yalikuwa sio rafiki kwa wanafunzi na walimu kutokana na upungufu wa matundu 20 ya vyoo na vyumba vya madarasa 8.
‘’Kwakweli kulikuwa na changamoto sana wanafunzi walikua wengi na madarasa machache lakini kwasasa hatuna watoto wanaokaa chini na msongamano wa wanafunzi darasani umepungua kwa kiasi kikubwa ,naishukuru serikali na Jafo kwa kutilia mkazo ukarabati wa miundombinu ya shule yetu’’ amesema
Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Ally Mohamed Swalehe ameishukuru serikali kwa kuboresha miundombinu ya shule hiyo rafiki kwa kuwa itaongeza ufaulu katika mitihani na kuepusha magonjwa ya milipuko shuleni hapo.
Sign up here with your email