MTOTO AMUUA BABA YAKE NA KUTAKA KUMFUKIA - Rhevan Media

MTOTO AMUUA BABA YAKE NA KUTAKA KUMFUKIA

Jeshi  la Polisi mkoani Ruvuma linamshikilia Patrick Malindisa (29) mkazi wa Mtaa wa Namanyigu Manispaa ya Songea kwa tuhuma za kumuua baba yake mzazi Athanasi Malindisa (70) kwa kumpiga na kitu chenye ncha kali kichwani na kidevuni na kisha kutaka kuufukia kwenye shimo alilochimba ndani ya nyumba yao.

Mmoja wa wanafamilia ambaye ni mdogo wa marehemu Pius Malindisa jana  alisema walipata taarifa ya kifo cha ndugu yao Januari Mosi mwaka huu saa 1:30 jioni  kutoka kwa mtoto wa marehemu Patrick Malindisa.

Alisema marehemu alikuwa akiishi na mtoto wake huyo ambapo baada ya kufanya mauji hayo alianza kuwaarifu ndugu kuwa amefariki kwa ugonjwa wa tumbo.

Kutokana na taarifa hizo ndugu walikusanyika nyumbani kwa marehemu ambapo baada ya kuingia ndani walikuta akiwa amelala ndipo walipowaita viongozi wa mtaa na baada ya kufunua walibaini marehemu ameuawa kwa kupinga na kitu chenye ncha kali kichwani na kidevuni.

“Baada ya kufanyika kwa uchunguzi wa awali tulitoa taarifa polisi ambapo walifika na kuuchukua mwili kwa uchunguzi zaidi. Na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma huku mtoto wake akishikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi.

“Tulipofika hapa tulikuta shimo limechimbwa ndani ya nyumba na inaelekea lilimshinda na kuamua kuanza kutoa taarifa kwetu ambapo alidai alikuwa anaumwa ugonjwa wa tumbo,” alisema Pius

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo ambapo kwa sasa wanamshikilia mtoto wa marehemu, Patrick Malindisa kwa uchunguzi zaidi.
Previous
Next Post »