MTEULE WA JPM ABEBESHWA TUHUMA - Rhevan Media

MTEULE WA JPM ABEBESHWA TUHUMA

John Magufuli, Rais wa Tanzania (kulia) akiwa na Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam

MTEULE wa Rais John Magufuli anatajwa kuwa kikwazo katika ujenzi wa jengo la kitegauchumi lililopo Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, 
Ni Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye amebebeshwa tuhuma hizo leo wakati wa kikao cha Baraza Kuu la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) Taifa,kilichofanyika mjini Dodoma.
Suleiman Kikingo, Mwenyekiti wa TALGWU, ndiye aliyetoa tamko hilo katika utangulizi wake wa kumkaribisha Jenista Mhagama, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana Ajira na Watu wenye Ulemavu aliyekuwa ngeni rasmi.
Mbali na tuhuma hizo, TALGWU wamesema Makonda amekuwa na tabia ya kujifungia ofisini na kufanya maamuzi badala ya kukutana na viongozi wa chama hicho kwa mazungumzo ya namna bora ya kuendeleza jengo hilo.
Kikingo amesema wangependa serikali iingilie kati suala hilo lililosababishwa na Makonda kabla ya wao kuchukua hatua stahiki.
Amesema Makonda amesimamisha ujenzi wa jengo hilo la kitegauchumi kwa uamuzi wa peke yake akishindwa kushirikisha uongozi wa TALGWU kama alibaini tatizo lolote kwenye ujenzi huo.
“Tunaiomba serikali kuhakikisha inaingilia kati suala hili maana linaonekana kutugawa sisi viongozi… hatukuwepo wakati mkuu wa mkoa akitoa hoja ya ukaguzi wa viwango vya ubora wa jengo.
“Baada ya kupata taarifa za hatua yake, tumewasilisha nyaraka zote lakini bado ameendelea kukaa kimya na tulitarajia jengo liwe limekamilika kati ya Machi na Aprili mwaka jana.
“Lakini kwa uvivu wa kutekeleza majukumu yake au chuki binafsi, amezidi kukwamisha mradi na sasa chama chetu kujikuta kikiingia katika hasara kwani tunalipa mkopo wenye riba ambayo inatakiwa kutolewa kutokana na jengo kuchelewa kumalizika,” amesema.
Amesema pamoja na juhudi zao kutaka ufumbuzi wa mkwamo wa ujenzi, bado Makonda amegoma kukutana na viongozi.
“Amekuwa akitugandisha ofisini kwake toka saa 2 asubuhi hadi saa 12 jioni huku zikitolewa taarifa kuwa hayupo ofisini wakati tunajua yupo.
“Sisi viongozi tumekuwa tukitoka Arusha na mwingine Mtwara lakini tunapoteza nauli ambayo ni michango ya wanachama bila ya lililokusudiwa kutekelezwa,” amesema.
Kwenye mkutano wa Baraza Kuu TALGWU, waziri Mhagama amesema atalibeba jukumu hilo kwa nia ya kutatua na kukiwezesha chama hicho kukamilisha mradi wake.
Amesema kuwepo kitegauchumi kwa taasisi yoyote ile ni jambo jema kwa wanachama wake kwa kuwa ni sehemu muhimu ya kujenga nguvu ya kiuchumi ya taasisi husika.
“Kama chama kitakuwa na kitegauchumi chake, kitaweza kupunguza matatizo ambayo wanachama na watumishi wa umma wanakutana nayo kwa kunyanyaswa na taasisi za kifedha zinazojifanya kuwasaidia kumbe zinawakamua,” amesema waziri Mhagama.
Previous
Next Post »