MALALAMIKO ya wananchi kwamba, maisha yamekuwa magumu, sasa yamethibitishwa na serikali,
Dk. Philipo Mipango, Waziri wa Fedha na Mipango akizungumza na wahitimu wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP) katika mahafali ya 33 yaliyofanyika chuoni hapo mjini Dodoma, amethibitisha ugumu wa maisha wa sasa.Kauli ya Dk. Mpango ilijielekeza katika maisha ya watu wa vijijini ambapo amesema, kwa mujibu wa takwimu zilizofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, watu 100 wanaoishi vijijini kati yao watu 33 hawapati mahitaji yao muhimu.
Amesema wanaoishi mijini, watu 100 kati ya watu 22 hawapati mahitaji yao ya msingi na katika Jiji la Dar es Salaam watu wanne kati ya 100 hawapati mahitaji yao ya msingi na mtu mmoja kati ya watu 100 Dar es Salaam hapati chakula cha kutosha.
Kutokana na hali hiyo, amewataka wahitimu wa chuo hicho kuhakikisha wanatumia elimu yao waliyoipata kwa ajili kuwapatia wananchi maendeleo hususani waishio vijijini.
Amesema, iwapo wahitimu hao watatumia elimu waliyoipata kwa manufaa ya wananchi, ni wazi wataondokana na msemo ambao unatumiwa na vijana kwa kukimbilia mjini kwa madai kwamba, watabanana huko huko (mjini).
Hata hivyo, amewataka wahitimu hao kufanya kazi kwa uamifu, kujiepusha na vitendo vya rushwa pamoja na mambo ambayo yanaweza kuliingiza Taifa katika machafuko.
Prof. Razack Lokina, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa chuo hicho amesema, chuo kinakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Ametaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na kukosekana kwa mabweni ya wanafunzi wa kike jambo ambalo linasababisha wanafunzi kupanga mitaani na kujikuta wakipoteza maadili.
Sambamba na hilo amesema kutokana na uhaba huo wa mabweni, chuo kinapanga nyumba za taasisi za serikali au watu binafsi jambo ambalo linasababisha kuwepo kwa gharama kubwa za uendeshaji.
Changamoto nyingine ni kukosekana kwa jengo la utawala ambalo linakidhi viwango ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa uhaba wa wahadhiri.
Sign up here with your email