JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema lilimkamata Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Maombezi (GRC), Antony Lusekelo, maarufu kwa jina la Mzee wa Upako kwa mahojiano ya kawaida na kisha kumwachia.
Kauli hiyo ilitolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, ofisini kwake jana.
Sirro alitoa majibu hayo baada ya kuulizwa na waandishi wa habari kuhusu uchunguzi uliokuwa unaendelea dhidi ya Mzee wa Upako, aliyekamatwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwa tuhuma za kuwatukana baadhi ya majirani zake.
“Tulimkamata kwa mazungumzo ya kawaida,” alisema Sirro kwa kifupi.
Waandishi walipoendelea kuhoji nini kilichobainika baada ya mazungumzo na uchunguzi ambao Sirro aliliambia MTANZANIA Jumamosi wiki iliyopita kuwa ikibainika kuna kosa hatua za kisheria zitachukuliwa, alijibu tena kwa kifupi: “Tulikuwa na mazungumzo ya kawaida na hakuna kingine,” kisha aliaga: “Tumemaliza kwaherini.”
Majibu ya Sirro yameibua maswali kwa sababu hakufafanua iwapo Mzee wa Upako hana hatia na kwamba upelelezi wa tukio hilo uliohusisha majirani waliohojiwa uliishia wapi.
Jumapili iliyopita akiwa kanisani kwake Ubungo Kibangu, Mzee wa Upako alielezea mkasa uliotokea na kudai matusi aliyokuwa akitukana yapo katika Biblia, huku akilitupia lawama Jeshi la Polisi kuwa lilimhoji kwa hila.
Mzee wa Upako alikamatwa na Polisi wa Kituo cha Kawe baada ya majirani zake kutoa taarifa kuwa amewazibia njia na kurushiana maneno na majirani zake kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa tatu asubuhi, huku akidaiwa kuwa wakati tukio hilo linatokea alikuwa amelewa.
Sign up here with your email