Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema
Serikali ipo mbioni kupunguza muda wa utoaji wa leseni za biashara
nchini ili kutoa fursa kwa wananchi wengi zaidi kupata leseni hizo kwa
ajili ya shughuli za kibiashara.
Makamu
wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam
katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere wakati
anafungua mkutano wa wadau wa kuendeleza maeneo tengefu ya viwanda vya
usindikaji wa vyakula nchini.
Makamu
wa Rais amesema mpango utaenda pamoja na kupunguza baadhi ya kodi na
tozo ambazo ni kero kwa wananchi hasa wenye viwanda kama hatua ya kukuza
biashara na uwekezaji katika sekta ya viwanda nchini.
Amesisitiza
kuwa Serikali inaendelea na mazungumzo na wenye mabenki hususani benki
ya TIB ili kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wawekezaji wenye nia ya
kuanzisha viwanda.
Kuhusu
usindikaji wa bidhaa nchini, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye
pia ni Mjumbe katika jopo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa la
kumuwezesha mwanamke kiuchumi akiwakilisha nchi za ukanda wa Kusini na
Mashariki mwa Afrika amepongeza jitihada zinazofanywa na wasindikaji
wadogo nchini katika utengenezaji wa bidhaa mbalimbali ambazo zitakidhi
katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Serikali
inafarijika sana kuona kuwa wasindikaji wadogo nchini wamethubutu na
wana uwezo wa ushindani katika biashara ya ndani na hata nje, hivyo
tunayohaki ya kujigamba kwa kuthubutu, Tumeweza na Tuendelea Kusonga
mbele”
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema
umefika wakati kwa Wizara na taasisi za Serikali na wadau wa maendeleo
kuona umuhimu wa kuhakikisha viwanda vinajengwa vijijini ili mkulima
mdogo anapolima awe na uhakika wa kupata soko katika viwanda hivyo.
Amesema
kuwa hali hiyo itaondoa changamoto ya kusafirisha bidhaa nyingi ambazo
zinaharibika njiani au zinapofika sokoni na hivyo kukosesha jamii kipato
kilichotarajiwa.
Makamu
wa Rais pia amehimiza watafiti nchini wajielekeza katika kufanya tafiti
ambazo zitasaidia sekta binafsi na serikali kwa ujumla kuhusu namna
bora ya kukuza sekta ya viwanda nchini.
Kwa
upande wake, Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage
amekiri kuwa bado kuna changamoto kubwa ya maeneo ya yatakayojengwa
viwanda na kwamba Serikali imeliona tatizo hilo na inalifanyia kazi
ambapo tayari imeshaziagiza Halmashauri zote nchini kujenga maeneo kwa
ajili ya viwanda.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es Salaam
Sign up here with your email