Mkuu wa Chuo cha Taifa cha
Usafirishaji (NIT), Prof. Zakaria Mganilwa akitoa taarifa ya utendaji wa
chuo hicho kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame
Mbarawa katika uzinduzi wa Baraza la Chuo hicho, jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti mpya wa Baraza la Chuo
cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Prof. Bavon Nchomba akifafanu jambo
kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa
katika uzinduzi wa Baraza la Chuo hicho, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza na wajumbe wa Baraza la
Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), katika uzinduzi wa Baraza jipya
la Chuo hicho, jijini Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa Chuo cha Taifa cha
Usafirishaji (NIT), wakisikiliza hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa katika uzinduzi wa Baraza jipya la
Chuo hicho, jijini Dar es Salaam.
………………………………………………………………………………………
Chuo cha Taifa cha Usafirishaji
(NIT), kimetakiwa kuchangamkia fursa za kuandaa wataalam wa kada
mbalimbali za usafirishaji wa anga ili kuinua sekta hiyo na kuiwezesha
nchi kujulikana Kimataifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam
katika uzinduzi wa Baraza la Chuo hicho, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa kuzalisha wataalam pekee
haitoshi bali ni jukumu la uongozi wa Baraza hilo kuhakikisha
wanawasaidia wataalam hao kwa kuwaunganisha na mashirika makubwa ya
usafirishaji lengo ni kuwajengea uwezo na kuwatambulisha kimataifa.
“Tayarisheni wataalamu na
muwakutanishe na Wakurugenzi wakuu wa Makampuni kama Emirates, Qatar na
Etihad ili kuwawezesha kupata fursa kirahisi na wao kuweza kuonekana
kimataifa”, amesema Profesa Mbarawa.
Ameongeza kuwa Chuo kinahitaji
kuchukua wafanyakazi kutoka Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), ili kutoa
mafunzo kwao kwa ajili ya kuzalisha wataalam wenye ujuzi na uwezo wa
kujenga miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (Standard
Guage).
“Msipotumia fursa kama hizi za
kuandaa wataalamu wa mbalimbali, tutakosa watalaamu wazawa wa miradi
mikubwa na kuanza kulalamika kuwa Chuo kipo lakini hakithaminiki kumbe
mwanzoni tulishindwa kujipanga”, amefafanua Waziri Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amelipongeza baraza
lililopita kwa uwezo mkubwa wa kukusanya mapato ya ndani yatokanayo na
ada za wanafunzi kutoka Bil. 2.1 kwa mwaka wa fedha 2011/2012 hadi
kufikia Bil. 5.1 mwaka 2015/2016.
Aidha, Prof. Mbarawa ameutaka
uongozi wa Chuo hicho kuweka mifumo imara ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA), ili kuweza kuwajengea mazingira mazuri kati ya
Walimu na Wanafunzi.
Sambamba na hilo, ameutaka
uongozi kupunguza idadi ya kozi zinazotolewa chuoni hapo na kuwa na kozi
chache zenye tija na soko kimataifa ili kukifanya chuo hicho kuwa cha
kipekee Afrika.
Kwa upande wake Mwenyekiti mpya
wa Baraza hilo Prof. Bavon Nchomba amemhakikishia Waziri huyo
kushughulikia changamoto zote zinazoikabili chuo hicho kwa kuanzia na
upunguzaji wa idadi za kozi zisizo na tija.
Naye, Mkuu wa chuo hicho Prof.
Zakaria Mganilwa amesema chuo hicho kitaendelea kuandaa wataalamu mahiri
na waliobobea katika Sekta ya Uchukuzi na Usafirishaji na kuomba
Serikali kuendelea kusaidia kuboresha miundombinu ya chuo hicho.
Sign up here with your email