RAIS Dk. John Pombe Magufuli amekubali na kuridhia ombi la kusitisha mkataba na kustaafu kwa Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna (CGP), John Minja, kuanzia jana.
Kutokana na ombi hilo, Dk. Magufuli amemteua Dk. Juma Malewa kuwa Kaimu Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini hadi hapo uteuzi wa Kamishna Jenerali wa Magereza utakapofanyika.
Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu na kusainiwa na Mkurugenzi wake, Gerson Msigwa, ilieleza kuwa, mbali na kukubali ombi hilo, Dk. Magufuli pia alimpongeza Kamishna Minja kwa utumishi wake na kumtakia maisha mema ya ustaafu.
Jumanne wiki hii Dk. Magufuli alifanya ziara katika Gereza la Ukonga, Dar es Salaam, ambako alitumia nafasi hiyo kupiga marufuku uuzwaji wa sare za majeshi nchini na watu binafsi na kutaka wote wanaofanya biashara hiyo kukabidhi kwa majeshi husika mara moja.
Rais Magufuli alipiga marufuku hiyo kufuatia maelezo kutoka kwa baadhi ya askari wa Jeshi la Magereza kuwa wamekuwa wakinunua sare za jeshi hilo kutoka kwa watu binafsi, kinyume cha taratibu za majeshi nchini.
Pia alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua mara moja wale wote watakaobainika kuuza sare za majeshi nchini.
Sign up here with your email