MALALE HAMSINI OUT JKT RUVU, IN RUVU SHOOTING - Rhevan Media

MALALE HAMSINI OUT JKT RUVU, IN RUVU SHOOTING





UONGOZI wa timu ya Ruvu Shooting umeingia kndarasi na Kocha Malale Hamsini kuifundisha timu hiyo kipindi cha mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Vodacom, Tanzania Bara baada ya kubwagiwa manyanga na ndugu zao JKT Ruvu.

Kocha Malale tayari amewasiri kambini Mabatini ambapo Jumatatu, Desemba 5, 2016 ataanza rasmi majukumu aliyokabidhiwa ya kukinoa kikosi hicho kama Kocha mkuu.

Uongozi wa Ruvu Shooting umesema, umefikia maamzi ya kumchukua kocha Malale kutokana na uwezo wake mzuri wa kufundisha mpira kama unavyopambanuliwa na mafanikio makubwa katika timu alizowahi kuzifundisha.

"Malale ni kocha mzuri sana, ameifundisha timu ya JKU kwa mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuipandisha hadi ligi kuu ya Zanzibar mwaka 2013, msimu wa 2014 ikiwa mikononi mwake ilishika nafasi ya pili katika ligi hiyo ya Zanzibar, aliifikisha timu hiyo nusu fainali ya mashindano ya kombe la Mapinduzi, pia aliiwezesha kutwaa ubingwa wa mashindano ya majeshi mwaka 2013 Jijini Dar es salaam" wamesema.

Waliongeza kwamba, mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara, msimu wa 2015/16 alikwenda kuifundisha Ndanda FC ambayo ilimaliza mzunguko wa kwanza wa ligi ya msimu huo ikiwa ya pili kutoka mwisho lakini akaiwezesha timu hiyo kumaliza ligi ikiwa nafasi ya saba!

Aidha uongozi wa Ruvu Shooting ulisema kwamba, Malale akiwa na timu ya JKT Ruvu msimu huu wa ligi, mbali na timu hiyo kutokuwa katika nafasi nzuri ya msimamo ameiwezesha timu hiyo kuonesha ubora wa kucheza mpira wa kufundishwa.

"Tunaimani Malale ni kocha mzuri, kwa ushirikiano wake na msaidizi wake Seleman Mtungwe ambaye naye ni kocha bora mwenye viwango, timu yetu itakuwa imara na bora zaidi, itakuwa tishio na tutafanya vizuri mno katika msimu huu wa ligi" walisema Ruvu Shooting.

Malale pia ni kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, alianza rasmi kazi ya ukocha mwaka 2004 akiifundisha kwa mafanikio makubwa timu ya Ngome ya Fuoni na baadaye timu ya Faru ya Jumbi.


Previous
Next Post »