LEMA AWATAKA MAWAKILI WAMUACHE ASOTE RUMANDE - Rhevan Media

LEMA AWATAKA MAWAKILI WAMUACHE ASOTE RUMANDE


godbless-lema

MBUNGE wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, amewataka mawakili wake kutofanya uamuzi wowote baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kufuta rufaa ya maombi ya dhamana yake.
Akizungumza jana na familia, viongozi na wafuasi wa Chadema wakati anakwenda kupanda gari kurudi mahabusu, aliwataka wasiogope na wasijihusishe na chochote, bali waiache Jamhuri imalize kazi yake.
“Msiogope, jitieni moyo, nimewaambia msijihusishe na chochote hadi pale Jamhuri itakapomaliza kazi yake,” alisema Lema, ambaye yuko mahabusu kwa muda wa mwezi mmoja sasa katika Gereza Kuu la Kisongo.
Naye Wakili John Mallya aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamezungumza na Lema baada ya mahakama kutoa uamuzi huo na amewaomba kutojishughulisha na suala lolote la kukata rufaa, ingawa wao kama mawakili wanaona bado kuna njia za kufanya hivyo katika mahakama za juu.
Alisema Lema amewaambia atakaa mahabusu gerezani Kisongo bila shida na kuhusu hoja kwamba walikata rufaa nje ya muda, alisema wao wanafahamu ni ndani ya muda, ila mahakama ikishatoa uamuzi wake hawawezi kukataa, lazima wakubaliane nayo, hivyo watakutana ili kupanga mbinu za kumpigania apate haki yake ya dhamana.
“Tumezungumza na mteja wetu ametuelekeza kwamba ingawa tuna njia ya kwenda katika Mahakama ya Rufaa au kufanya mapitio katika Mahakama Kuu na ngazi nyingine za juu za mahakama hii, ametuambia tuache, yeye atakaa magereza Kisongo kwa idhini yake, mchana wa leo (jana) mawakili tutakutana tujue tunafanyaje,” alisema Mallya.
Akisoma uamuzi wa kufuta maombi ya rufaa ya dhamana ya Lema, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Angero Rumisha, alisema mahakama hiyo imeifuta rufaa hiyo kwa sababu wakata rufaa waliikata nje ya muda.
Rumisha alisema waomba rufaa walitakiwa kuwasilisha kusudio la kukata rufaa ndani ya siku 10 tangu uamuzi wa maombi ya marejeo ya mwenendo na uamuzi wa mahakama ya chini kutupwa Novemba 11, mwaka huu na Kaimu Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Sekela Moshi.
Alisema kutokana na sababu hizo, mahakama hiyo inakubaliana na pingamizi la awali lililowasilishwa na mawakili wa Serikali, Paul Kadushi na Matenus Marandu, walioomba mahakama hiyo isisikilize rufaa hiyo kwa sababu imekiuka matakwa ya sheria yanayotaka kutolewa kwa kusudio la kukata rufaa kabla ya rufaa yenyewe.
“Rufaa ilikuwa nje ya muda, iko kiharamu mahakamani na hawakutoa notisi ya nia ya kukata rufaa, hivyo Jaji anakubaliana na pingamizi la mawakili wa Serikali na anaifuta rufaa ya Lema,” alisema Rumisha.
Novemba 28, mwaka huu, rufaa hiyo ilipangwa kusikilizwa kwa Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Fatuma Masengi, lakini ilishindikana baada ya mawakili wa Serikali kuweka pingamizi chini ya Kifungu cha 361(1) (a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kama ikivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.
Walidai mahakamani hapo kuwa, mawakili wa Lema wamekiuka matakwa ya sheria yanayowataka kutoa notisi ya nia ya kukata rufaa badala ya kukata rufaa yenyewe na pingamizi hilo kusikilizwa kwa njia ya maandishi na Novemba 30, mwaka huu mawakili wa pande zote mbili waliwasilisha hoja zao mahakamani hapo.
Lema alikuwa akiwakilishwa na mawakili Mallya, Adam Jabir, Sheck Mfinanga na Fzraji Mangula, huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Kadushi na Marandu.
Awali, kabla ya Rumisha kutoa uamuzi huo, Jabir aliiomba mahakama hiyo impe Lema nafasi ya kuzungumza, lakini alimtaka asubiri uamuzi huo usomwe.
Baada ya Rumisha kumaliza kusoma uamuzi huo, alimpa nafasi azungumze anachotaka kusema mteja wake au mawakili wake watoke ndipo Lema azungumze, ambapo Jabir alidai kuwa, mteja wake amekuwa akilalamika ndugu na wafuasi wake kukatazwa kuingia mahakamani wakati kesi hiyo inasikilizwa katika mahakama ya wazi.
“Anaomba ndugu zake na wafuasi waruhusiwe kuingia japo wamuone Lema, hoja hii imeshazungumzwa zaidi ya mara tatu na askari walipewa maelekezo wakague watu na kuwaruhusu kuingia, ila hata hawa unaowaona wameingia mahakamani kwa nguvu, wengine wanawake wanakaguliwa na askari wa kiume, wananyanyaswa,” alidai Jabir.
SEHEMU YA MABISHANO YAO YALIKUWA KAMA IFUATAVYO
Rumisha: Mahakama inaendesha shauri hili katika mahakama ya wazi, hakuna mtu anayezuiliwa kuingia, hata kama si ndugu yake, changamoto ninayoona hapo nadhani ni udogo wa hiki chumba.
Jabir: Ni bora waingie mahakamani hata wakikaa pale nje
Rumisha: Wakikaa nje itasaidia nini?
Jabir: Nakumbuka Lema alikuwa na kesi ya ubunge (uchaguzi) katika mahakama hii na mahakama iliweka spika nje na watu wakawa wanasikiliza hata wakiwa nje ya chumba cha mahakama.
Rumisha: Kesi za ubunge zina fedha yake kwa ajili ya kuziendesha, watu wanakuwa ni wengi na spika zinakodishwa, unataka fedha nitoe wapi? Fedha inayotolewa iko katika bajeti, natamani tungekuwa na fedha tungejenga ukumbi mkubwa wa mahakama.
Baada ya majibizano hayo, Jabir, alimuomba Rumisha ampe Lema nafasi azungumzie jambo hilo, lakini aliwaeleza kuwa kama wanataka azungumze itabidi mawakili wake watoke nje na mawakili hao waliposimama kutaka kutoka nje aliweka karatasi mezani na kusema kesi imekwisha na Lema akashindwa kuzungumzia suala hilo.
MKE WA LEMA
Neema Lema ambaye ni mke wa Lema, akiwa na watoto wake wawili mahakamani hapo, alisema wamekubaliana kutofungua kesi yoyote hadi hapo Jamhuri  itakapoona inafaa na akaongeza kuwa, wanachofahamu wao ni kwamba Tanzania hakuna mwenye hati miliki, iwe kiongozi yeyote mwenye cheo chochote watapita na maisha yataendelea.
“Nashukuru watu wote waliojitokeza kuja katika kesi hii, licha ya usumbufu mwingi waliokutana nao lakini hawakukata tamaa, kama familia na nilipoongea na mume wangu Lema tumeona kuwa katika kesi hii kuna mtu anataka mahakama ifuate maagizo yake, hivyo na sisi tumeona aachwe huyo mtu yafuatwe maagizo yake na afanye atakalo,” alisema Neema.
Naye baba mzazi wa Lema, Mzee Jonathan Lema, akizungumza kwa uchungu, alisema anaona uamuzi wa hakimu umeingiliwa kwa sababu kosa la mtoto wake lina dhamana na mahakama iliamua kumpa dhamana, ila kila hatua wanayochukua wanawekewa vizingiti.
“Tumeona kama familia tuache Lema akae ndani, tunamwachia Mungu afanye kazi yake, kwa sababu kila tufanyalo linaingiliwa,” alisema Jonathan.
Kwa upande wake, Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, alisema kama chama kimesikitishwa na mwenendo wa kesi hiyo tangu mwanzo na kudai kimefedheheshwa kwa sababu zaidi ya mara tatu mahakama hiyo imekuwa ikitoa maelekezo juu ya mahakama hiyo ya wazi inaruhusu watu wote wahudhurie, lakini haki ya mbunge na wapiga kura wake wamekuwa wakivunjiwa kwa kuzuiwa na kutishwa na askari.
Awali, Mawakili wa Lema wakiongozwa na Peter Kibatala, walikata rufaa namba 112/113 ya mwaka 2016 katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, ili kudai haki ya dhamana aliyonyimwa kutokana na makosa ya kisheria yaliyofanya na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
Novemba 8, mwaka huu, Lema alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, akikabiliwa na kesi mbili za uchochezi na alishindwa kupata dhamana kutokana na maombi ya mawakili hao wa Serikali waliodai kuwa anakabiliwa na kesi nyingine mbili za uchochezi katika mahakama hiyo, hivyo asipewe dhamana kwa kuwa alipopewa dhamana kwa kesi hizo bado alirudia kufanya makosa kama hayo.
Wakili Kadushi aliwasilisha kwa njia ya mdomo kusudio la kukata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ya kupinga uamuzi wa mahakama hiyo kumpa Lema dhamana, uliotolewa na mahakama hiyo, lakini haukutekelezeka kwa sababu ya nia ya kukata rufaa waliyoitoa.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi, Marandu alisema walishindwa kuwasilisha sababu za wao kukata rufaa Mahakama Kuu kutokana na maombi ya marejeo ya mwenendo na uamuzi wa mahakama ya chini yaliyoombwa na mawakili wa Lema.
“Tuliweka notisi ya nia ya kukata rufaa, ila tulishindwa kwenda Mahakama Kuu kukata rufaa hiyo na kutaja sababu za rufaa, tuna siku 45 za kukata rufaa, ila tulishindwa kwa sababu upande wa utetezi walipeleka maombi Mahakama Kuu, tusingeweza kufanya mambo mawili kwa wakati mmoja, ila upande wa utetezi usipokuja na kitu kingine rufaa tutaipeleka Mahakama Kuu, sisi hatuna nia ya kuchelewesha suala hili,” alisema Marandu.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, amemtembelea Lema gerezani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Msemaji wa ACT-Wazalendo, Abdallah Khamis, Zitto alimtembelea Lema saa 11 jioni jana gerezani Kisongo.
“Leo (jana) Ijumaa nimepata fursa ya kumsalimu Lema. Nimemtembelea kama mbunge mwenzangu na kumhakikishia solidarity (mshikamano) katika harakati za kutafuta na kulinda haki.
“Lema ana ari kubwa ya mapambano. Anasikitishwa sana na ukiukwaji mkubwa wa haki na mahakama kuonekana kuendeshwa na Serikali. Yeye ameona ni bora akae ndani hadi hapo dola itakapopenda kumpa dhamana. Kosa lake lina dhamana na hakimu alimpa dhamana,” alisema Zitto kupitia taarifa hiyo.
Pia Zitto alisema Lema ameomba tutazame mahabusu wengi wanaokaa ndani miaka mingi bila kesi zao kuendelea.
“Tuwatetee. Amemshukuru Mungu kwa kumpa mke jasiri anayempa moyo na ndiyo ngome yake kwa sasa. Nimemwomba Lema aone kuwa haya mapambano si yake peke yake, bali anawakilisha watu wengi wanaotaka haki kutendeka katika uendeshaji wa nchi yetu. Siku zote haki hushinda,” alisema Zitto.
Lema alikamatwa Novemba 2, mwaka huu nje ya Viwanja vya Bunge, mjini Dodoma, wakati anahudhuria vikao na hadi sasa haijulikani ataletwa lini mahakamani kuendelea na kesi hiyo, huku watumishi wa mahakama wakitarajiwa kwenda likizo kuanzia Desemba 15, mwaka huu na kutarajiwa kuanza kazi zake mwakani.
Previous
Next Post »