MKUU wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa ,Said Mtanda amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo , Julius Kaondo kuhakikisha inamsaka, kumkamata na kumfikisha mahakamani ‘mvamizi’ anayendelea kuishi kwa kificho ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Mfili.
Mtanda, alitoa agizo hilo mbele ya Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula alipokutana na watumishi wa halmashauri hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita.
“Ninazo taarifa, licha ya operesheni tuliyoifanya siku tatu kuwaondoa wavamizi waliokuwa wakiishi na kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya msitu huu, bado yupo mtu amejificha na anaendelea kuishi ndani ya msitu huo ….
Sasa namwagiza mkurugenzi mtu huyo asakwe, akikamatwa hakikisha
anafikishwa mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake,”alisisitiza .
Alisema ni marufuku kwa mtu yeyote kuishi na kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya msitu huo na atakayekaidi atajutaa yake .Alisisitiza kuwa msitu huo ni eneo oevu umehifadhiwa kihalali kupitia sheria ndogo ya mwaka 1998 .
Alisema mwezi uliopita aliongoza operesheni maalumu ambapo wavamizi wote waliokuwa waiishi kinyume cha sheria katika msitu huo, waliondolewa, huku nyumba na mashamba vikiteketezwa kwa moto .
Naibu Waziri,Angelina aliwataka wananchi kuhakikisha msitu huo, unalindwa kwa sababu ni chanzo pekee cha maji kinachotegemewa na wakazi wa mji wa Namanyere.
Sign up here with your email