Najiamkia asubuhi nikiwa bukheri wa afya, huku nikiwa nimepata mapumziko mazuri ya weekend, sanjari na kupata fursa ya kuwajulia hali ndugu zangu wa Kariakoo na kuhudhuria mikutano ya kidini na maulid Jumapili hii kule Msaasani kwa swahiba wangu Zingizi.
Kama ilivyo ada baada ya kufanya mazoezi kidogo na kuunyosha mwili napitia taarifa za magazeti ya leo kwenye television...Napatwa butwaa tena kuona porojo zimetamalaki katika baadhi ya magazeti.
Yapo yalioandika kuhusu Daniel Aggey kipa wetu mpya, kwamba eti kaugomea uongozi kuhusu usajili. Mengine ni kuhusu Mkude na Ajibu. Hawa imeripotiwa eti wamesajili Yanga na mengine yapo yaliyozungumzia MO kujitoa Simba.
Kwa kadri nnavyofahamu ni wajibu wa mwandishi kubalance story upande wa pili baada ya kupata hiyo story huko walipoikota.
Lakini kinachoonekana hizi story zinatungwa tu na baadhi ya waandishi ama kwa nia ya kuuza magazeti au kwa nia ya kutugombanisha na washabiki wetu. Na katika hili wapo wanaoamua kujitoa kimasomaso kwa kunipigia kutaka kubalance hizo porojo!!
"Vp kuhusu Ajibu kwenda Yanga unasemaje? Na tunaona picha ya Mkude na Msuva mitandaoni, twaambiwa ndio anampeleka Yanga. Je, Simba ina kauli gani?
Huwa naumia sana kuulizwa maswali ya aina hii. Yaani mtu anatunga story kisha mimi ndio nibalance. Huku ni kunikosea kulikopitiliza, na kuivunjia heshma klabu kulikochupa mpaka!!
Niwahakikishie wachezaji wote hao ni mali ya Simba na taarifa zote za kwenda Yanga au kugoma kusajili ni uongo MKUU unaofaa kupuuzwa kwa kiwango cha kupuuza uvumi wa mtu kugeuka chatu...
Na hili la MO kujitoa ni aina ya jambo la hovyo kabisa! Nnaongea na MO mara kwa mara. Sijui hawa waandishi nini hasa wanakitafuta kwa Simba?Halaf ukiisoma story, eti ni habari za ndani. Ndani? Ndani wapi, uvunguni?
Nitoe wito kwa wana-Simba tena na tena, taarifa za usajili au zozote zile nitatoa mimi au viongozi wa klabu na sio mwingine yoyote.
Zipuuzeni taarifa za kutengenezwa... Tukiwa na jambo tutwajulisha rasmi. Pia niwasihi waandishi wenzangu hasa wale watungao story, wanapoteza heshima yao na wanainajisi taaluma hii muhimu sana,
Kwangu mimi binafsi nitaendelea kushirikiana na wao kwa kila hali ili kwa pamoja tubaki na weledi na maadili ya kazi hii inayobeba mhimili huu mkuu wa nne wa nchi yetu.
Sign up here with your email