WATUMIAJI wa mabasi ya mwendo kasi wamerahisishiwa jinsi ya kulipia kadi zao za kusafiria, anaandia Pendo Omary.
Hatua hiyo imetokana na Kampuni ya Mawasiliano ya Simu za Mkononi ya Vodacom Tanzania kuingia ubia na Kampuni ya Maxcom Africa katika kuweza kuongeza salio kwenye kadi zao za kusafiria kupitia huduma ya M-Pesa.Huduma hii imeanza rasmi tarehe 1 Agosti 2016 na kuwalenga watumiaji wote wa mabasi ya mwendo kasi jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia huduma hiyo Sitoyo Lopokoiyit, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Huduma za Kifedha wa Vodacom Tanzania amesema, “M-Pesa imeongeza wigo zaidi na unafuu kwa watumiaji wa mabasi haya mbali na njia nyingine zilizokuwa zikutumika kama Mawakala wa MaxMalipo au kwenye vituo mbalimbali vya Mabasi ya Mwendokasi (DART).
“Ushirikiano kati ya Vodaco, Maxcom na DART ni muendelezo wa juhudi za kuhakikisha kwamba, huduma ya M-Pesa inaendelea kumrahisishia na kumboreshea maisha ya kila siku Mtanzania,” amesema Lopokoiyit.
Juma Rajabu, Mkurugenzi wa Maxcom Africa amesema “mfumo uliowekwa na MaxMalipo kwenye usafiri huu wa mabasi ya mwendo kasi ni mfumo wa kisasa na salama zaidi unaotumia kadi maalumu pamoja na tiketi zenye QR codes.
“Pia mfumo huu umeboreshwa zaidi kwa kuunganishwa na kampuni za mawasiliano kama Vodacom Tanzania ambapo wasafiri bila kupoteza muda, wanaweza kuweka salio katika kadi zao za kusafiria kupitia huduma iliyo bora na ya uhakika ya M-Pesa,” amesema Rajabu.
David Mgwassa, Mkurungezi Mkuu wa UDART amesema, matumizi ya kadi ni muendelezo wa utambuzi wa Tanzania, kwenye kuelekea maisha ya kisasa.
“Kadi ya DART inamsaidia abiria kuondoa kero ya kutembea na pesa taslimu na kupanga foleni kwani inamuwezesha kulipia nauli kabla ya safari. Uwezo wa kutumia simu yake ya mkononi unaondoa usumbufu wa kupanga foleni kwenye vituo vya mabasi ya mwendo haraka.
“Kizuri zaidi ni kwamba, kadi hii inaweza kujazwa kiwango chochote cha fedha kisichozidi shilingi 30,000 kwa wakati mmoja na haina muda wa kikomo wa matumizi na fedha inayokuwa ndani ya kadi itaendelea kuwemo kwenye kadi bila kikomo mpaka mhusika atakapoitumia,” amesema Mgwassa
Sign up here with your email