TRL YAZINDUA TRENI YA MIZIGO - Rhevan Media

TRL YAZINDUA TRENI YA MIZIGO

KAMPUNI ya Reli Tanzania (TRL) imezindua treni mpya ya kusafirisha mizigo, huku ikiwaasa wafanyabiashara kutumia treni hiyo kusafirisha mizigo yao ili kulinda ubora wa barabara.
Treni hiyo inayojulikana kama ‘Block Train’ jana iliwasili jijini Dar es Salaam ikitokea mkoani Mwanza ikiwa na mzigo wa pamba wa tani 757 ambako ilianza safari Jumatatu iliyopita.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wakati wa kupokea treni hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TRL, Shaban Kiko, alisema uzinduzi wa treni hiyo ni jitihada za kuhakikisha wanarahisisha usafirishaji wa mizigo.
Alisema ni muhimu kwa wafanyabiashara wanaosafirisha mizigo yao, kutumia treni hiyo ikiwa ni hatua muhimu kwani sekta ya reli ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi.
“Imekuja na mzigo wa tani 757, mzigo huo upo katika mabehewa 19, mabehewa mawili ni mzigo uliotokea Bukwimba, mabehewa tisa uliotokea Malampaka na mabehewa manane ni kutoka Mwanza,” alisema Kingo.
Alisema, kwa kipindi kirefu mabehewa ya kampuni hiyo yalikuwa yakipeleka mizigo mikoani na kurudi tupu jambo ambalo lilikuwa likisababisha hasara kwa kampuni hiyo. Alisema wafanyabiashara hawana budi kutumia treni hiyo kwa kuwa usafirishaji wake ni salama na pia gharama zake ni nafuu ikilinganishwa na usafiri wa njia ya barabara.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo imejizatiti katika kuhakikisha usafirishaji wa abiria na mizigo ndani ya Jiji na hata mikoani unakuwa ni kipaumbele chao cha kwanza.
Kiko alisema treni hiyo ni katika kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda, hivyo wamiliki wa viwanda wanaweza kutumia usafiri huo kusafirisha malighafi zao kwa njia hiyo.
Awali kampuni hiyo ilikuwa haisafirishi pamba kutokana na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiikabili, ikiwemo uchakavu wa miundombinu ya reli, ambazo kwa mujibu wa Kiko, zimeanza kufanyiwa kazi.
Alisema kwa sasa wamepata injini mpya ambazo wamezitengeneza katika karakana ya Morogoro na kwamba kipindi cha nyuma ilikuwa ikiwachukua muda mrefu wa wiki tatu hadi mwezi mmoja katika kusafirisha mizigo lakini sasa wanatumia muda mfupi.
Previous
Next Post »