SMZ KUAJIRI MADAKTARI PEMBA. - Rhevan Media

SMZ KUAJIRI MADAKTARI PEMBA.

WIZARA ya Afya imesema inakusudia kuajiri madaktari wapya katika Kisiwa cha Pemba kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la upungufu wa madaktari.
Naibu Waziri wa Afya, Harusi Said Suleiman, alisema hayo wakati alipotembelea Hospitali ya Wete na kupata taarifa ya kuwepo kwa tatizo la upungufu wa madakatari na kusababisha baadhi ya huduma kuzorota.
Alisema maandalizi ya ajira za madaktari kwa mwaka wa fedha 2016/2017 yamekamilika.
“Tunakusudia kuanza kuajiri madaktari katika mwaka wa fedha 2016/2017, ikiwa ni moja ya hatua ya kukabiliana na tatizo la upungufu wa madaktari,” alisema.
Hata hivyo aliwataka wazazi kusaidia tatizo hilo ambapo madaktari wengi wanapoajiriwa na kupelekwa Pemba huanza kutoa sababu mbalimbali wakitaka kurudishwa Unguja.
Alisema tatizo hilo ni kubwa zaidi kwa madaktari wanawake ambao huibua visingizio mbalimbali ikiwemo kurudi Unguja kuishi pamoja na waume zao.
“Hilo ndilo tatizo linaloikabili Wizara ya Afya kwa kuajiri madaktari wengi wanawake lakini baada ya miaka miwili huomba uhamisho kurudi Unguja kwa ajili ya kuishi na waume zao,” alisema.
Alisema tatizo la upungufu wa madaktari kwa upande wa Pemba litafikia mwisho baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Hospitali ya Abdalla Mzee iliyopo mkoani Pemba.
Alisema ujenzi wa hospitali hiyo unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China upo katika hatua ya mwisho ambapo kwa sasa mchakato unaofanywa ni matayarisho ya ajira za madaktari wa hospitali hiyo.
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China tangu mwaka 1968 imekuwa ikitoa madaktari bingwa kuja kufanya kazi katika hospitali hiyo ambayo hadi kukamilika kwake itakuwa na hadhi ya rufaa.
Previous
Next Post »