Hatimaye imethibitika kuwa mabaki ya ndege yaliyookotwa Kisiwani Pemba na mwananchi Chunguwa Hamad Chunguwa ni kweli mabaki ya ndege ya Shirika la Malaysia,B777 #MH370 iliyopotea Machi 08 2014 na kupoteza maisha ya zaidi ya abiria 300.
Mkurugenzi wa TCAA, Mr Hamza Johari anasema wamethibitishiwa kuwa mabaki hayo yamefanyiwa uchunguzi na kugundulika kuwa ni sehemu ya ndege ya Air Malaysia, hivyo Tanzania kuwa sehemu ya nchi iliyosaidia kuteguwa kitendawili cha upoteaji wa ndege hiyo, Mr Hamza anasema wanachosubiri kwa sasa ni taarifa rasmi toka kwa mamlaka ya anga ya Malaysia ambao tayari wanaendelea kuwasiliana nao ili kuweka wazi kwa dunia kuwa sehemu ya mabaki ya ndege hiyo iliyozua kitendawili yamepatikana Kisiwani Pemba katika Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mr Hamza anasema kwa uaminifu ulioonyeshwa na mvuvi Chunguwa Hamad Chunguwa kuyawasilisha mabaki hayo kwa kutoa taarifa kwa mamlaka mbalimbali na hatimaye kufanikisha kusafirishwa kwa mabaki hayo, TCAA imemzawadia mvuvi huyo shilingi milioni mbili za Kitanzania.
Chunguwa Hamad Chunguwa wa kisiwa cha Kojani, Pemba, Juni 20, 2016 akiwa katika shughuli zake za uvuvi alikutana na mabaki hayo yakimangamanga katika eneo la bahari ya Hindi. Kituo cha uchunguzi wa kupotea ndege hiyo kipo Australia.
Sign up here with your email