OFISA ELIMU ASIMAMISHWA KAZI . - Rhevan Media

OFISA ELIMU ASIMAMISHWA KAZI .



BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha limemsimamisha kazi Ofisa Elimu Msingi wa wilaya hiyo, Sara Kibwana kwa kushindwa kusimamia majukumu ya idara hiyo na kushindwa kuonesha umoja na mshikamano kwenye usimamizi.
Hatua hiyo imekuja baada ya walimu wengi wa shule za msingi kumlalamikia ofisa huyo kwa kile kinachodaiwa hatoi ushirikiano wa kutosha katika Idara ya Elimu pindi wanapomhitaji.
Akitoa tamko hilo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani lililofanyika mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Lembris Noha alisema wamefikia hatua ya kumsimamisha ofisa huyo kutokana na kubaini mapungufu waliyoyaona kwenye Idara yake ya elimu baada ya kupokea malalamiko ya muda mrefu.
Alisema kuanzia sasa ofisa huyo hapaswi tena kuendelea na kazi za idara hiyo na kwamba wanamuagiza Mkurugenzi amuandikie barua ya kumsimamisha kazi ili aweze kuendelea na majukumu mengine.
“Baraza hili limeamua kumsimamisha kazi ofisa elimu kwani amekuwa akilalamikiwa na walimu na pia hana ushirikiano wa kutosha hivyo tunamuagiza Mkurugenzi amtafutie majukumu mengine,” aliongeza Lembris.
Aidha Lembris aliwataka wataalamu na watendaji kuhakikisha wanakuwa na ushirikiano wa kutosha katika utendaji kazi kwani wengi wa watendaji wanakuwa na lugha mbaya hali ambayo inakwamisha maendeleo.
Katika hatua nyingine, aliwataka wakuu wa shule kutoa waraka wa uchangiaji wa chakula kwa wazazi kwani baadhi ya shule kukosa chakula shuleni kunatokana na kukosekana kwa waraka huo.
“Tumesikia kuwa baadhi ya shule wanafunzi hawali chakula shuleni hali inayochangia utoro, niombe tu wahusika wa idara ya elimu watoe waraka kwa wazazi mapema iwezekanavyo ili waanze kuchanga fedha za chakula,” aliongeza.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Tarakwa, Elihuruma Laizer alisema baraza hilo limefikia hatua ya kumsimamisha kazi ofisa elimu huyo kisheria kutokana na kupokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa walimu ndipo walipokaa na kuyapitia na kuchukua maamuzi hayo kisheria.
Diwani wa Kata ya Oldonyosambu, Raymond Leirumbe akichangia katika baraza hilo alisema mtumishi yeyote aliyewekwa kwa lengo la kutumikia wananchi wanapaswa kuheshimu kanuni na sheria zilizopo ikiwa ni pamoja na kutumika katika nafasi zao ipasavyo na sio vinginevyo.
Previous
Next Post »