MHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Julius Nyahungo, amewataka wazazi kuacha kuwapa watoto wao ambao ni wanafunzi simu za Smart, kwani zina mambo mengi yanayoharibu ufahamu wa watoto.
Alisema hayo jana wakati wa mahafali ya darasa la saba ya Shule ya Sekondari ya Ignesius inayomilikiwa na Kanisa Katoliki.
Alisema simu hizo hazijabeba mambo ya utamaduni wa kiafrika, badala yake zimekuwa zikiharibu akili na ufahamu wa watoto, jambo ambalo wazazi wanatakiwa kuangalia kwa umakini.
“Tamaduni za kiafrika zinahitaji vitu vya kujielimisha lakini simu hizo zimekuwa zikichangia watoto kutokuwa na maadili, jambo ambalo huathiri ufahamu wao na kupotoka,” alisema. Pia alisema wazazi wana wajibu wa kusimamia watoto kufanya shughuli za nyumbani na si kukaa sebuleni kuangalia televisheni muda wote.
Alisema kila mzazi anatakiwa kusimamia watoto wake wawe na maadili mema na kujifunza kazi nyingine ambazo zitakuwa na tija kwao, si kuwaacha watoto wafanye kile wanachotaka.
“Utakuta mtoto yuko nyumbani kutwa nzima yuko kwenye televisheni hawawezi kujifunza kitu kitakachowasaidia kwenye maisha, usidhani hapo unampenda sana mtoto bali unamharibu kwani atakosa misingi mizuri hapo baadaye,” alisema.
Alisema wanafunzi wenye maadili wamekuwa wakifika mbali hasa kwenye elimu zao kwani wanakuwa na nidhamu na maisha yao.
Sign up here with your email