SERIKALI imesema mchakato wa kutafuta amani nchini Sudan Kusini unashughulikiwa na Umoja wa Nchi za Pembe ya Afrika (IGAD) na Tanzania inasaidia mchakato huo.
Katika mchakato huo, katika nafasi ya kwanza, Tanzania inasaidia urejeshaji wa amani nchini humo na ilianza wakati mazungumzo ya IGAD yanaendelea katika ngazi ya serikali chini ya chama tawala cha SPLM nchini Sudan Kusini.
Hayo yalibainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga, wakati akizungumza na gazeti hili kuhusu hatua zinazochokuliwa na Rais John Magufuli kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo Sudan Kusini ni mmoja wa wanachama wake.
Balozi Mahiga alisema Rais Magufuli hajakaa kimya kwenye mgogoro huo, ambao chanzo kikuu ni ugomvi ulioanza ndani ya chama hicho kati ya Rais Salva Kiir na mwenzake Dk Riek Machar na hatimaye ukagusa serikali.
Akizungumzia sakata hilo, Balozi Mahiga alisema mzozo wa nchi hiyo ulikuwa unashughulikiwa na IGAD, na kwamba Tanzania na Afrika Kusini zikaombwa kupitia vyama vyao CCM na ANC, kuwapatanisha wanasiasa hao wawili kwa ngazi ya chama, huku IGAD ikiwapatanisha kwa ngazi ya kiserikali.
Alisema vyama hivyo viwili vilikubaliana na kuwaita viongozi hao wawili wa Sudan Kusini, kwenda jijini Arusha kwa ajili ya kupatanishwa na waliitikia mwito na mazungumzo yalikwenda vizuri na wakapatana.
“Vyama vilifanikiwa kuwapatanisha Kiir na Dk Machar, na wao wakasema wamekubaliana kichama na ikaonekana jambo hilo litasaidia kusukuma makubaliano ya kule Addis Ababa, Ethiopia ambako mazungumzo ya IGAD yalikuwa yanaendelea kiserikali,” alisema Balozi Mahiga.
Balozi Mahiga alisema mazungumzo hayo yalifanywa kipindi ambacho hata nchi hiyo ya Sudan Kusini haijaingia ndani ya EAC na kwamba baada ya kuingia, viongozi hao walisema wamefurahi wamerudi nyumbani.
Akizungumzia nafasi ya pili ya Tanzania kama Mwenyekiti wa EAC, Balozi Mahiga alisema, baada ya nchi hiyo kujiunga, viongozi wa nchi nne kati ya sita za umoja huo za Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda walikaa kuzungumzia hali ya nchi hiyo.
Alisema viongozi hao walikubaliana kuwa ikiwa jumuiya hiyo itaamua kufanya vikao vya kutafuta suluhu nchini Sudan Kusini, watapunguza umakini wa mazungumzo hayo ambayo tayari yalikuwa yanasimamiwa na IGAD.
“Wakuu wa nchi hizi nne waliona si vyema na EAC ianze vikao kuhusu Sudan Kusini ambaye tayari amekuwa mwanachama, tukashauriana tuunge juhudi za IGAD na za Umoja wa Afrika (AU), ili kuwe na umakini kuliko kuwayumbisha wanaopatanishwa,” alisema Balozi Mahiga.
Hata hivyo, aliongeza kuwa Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa EAC, ameitisha kikao cha wakuu wa nchi hizo kitakachokaa jijini Dar es Salaam Septemba 19, mwaka huu na kwamba katika kikao hicho watazungumzia pia suala la Sudani Kusini.
Mchakato wa amani wa Sudan Kusini, chini ya IGAD inayoundwa na nchi za Kenya, Uganda, Sudan Kusini, Djibout, Eritrea na Ethiopia unaungwa mkono na AU, UN na EAC.
Sign up here with your email