MWALIMU
Daniel Msalika (42) wa shule ya msingi Nyasosi, wilayani Bariadi, mkoa
wa Simiyu amefariki dunia katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando alikokuwa
amelazwa akitibiwa majeraha.
Majeraha
hayo yalitokana na kushambuliwa na baadhi ya wananchi kwa madai ya
kujihusisha kimapenzi na wanafunzi wa kike wa shule hiyo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Onesmo Lyanga aliwaeleza waandishi wa habari
jana ofisini kwake kuwa mwalimu huyo alifariki dunia Julai 31 mwaka huu
saa nane usiku.
Kamanda
Lyanga alisema kuwa siku ya tukio Julai 27 mwaka huu saa 6.30 usiku,
wananchi hao ambao idadi yao haijafahamika, walivamia nyumba ya mwalimu
huyo baada ya kupata taarifa kuwa kuna mwanafunzi ambaye amelala
nyumbani kwake, jambo ambalo halikuwa la kweli.
“Wananchi
hao walipata taarifa ya kuwa nyumbani kwa mwalimu kuna mwanafunzi
ambaye amelala humo hivyo walimvamia kwa kuvunja mlango na kuanza
kumshambulia kwa kutumia silaha mbalimbali za jadi na kumsababishia
majeraha makubwa sehemu za kichwani na usoni lakini binti waliyemkuta
kwake ni mwenye umri wa miaka 18 na siyo mwanafunzi,” alisema.
Alisema
kuwa baada ya uvamizi huo, mwalimu huyo alikimbizwa katika Kituo cha
Afya cha Isanga kupatiwa matibabu, lakini hali yake iliendelea kuwa
mbaya na kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza,
lakini alifariki dunia.
Kamanda alisema kifo chake, kimesababishwa na majeraha ya kushambuliwa huku tuhuma dhidi yake zikiwa si za kweli.
Alitoa
mwito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi huku
wakisisitiza kuwa wote watakaobainika kusababisha kifo hicho, sheria
itachukua mkondo wake.
Sign up here with your email