MAMLAKA
ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza kupanda
kwa bei ya mafuta kuanzia leo kutokana na mabadiliko ya bei katika Soko
la Dunia.
Bei hizo za jumla na rejareja kwa mafuta ya aina zote ya petroli, dizeli na taa zimepanda, ikilinganishwa na bei zilizotolewa mwezi uliopita.
Mkurugenzi
Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi alisema bei za reja reja, zimeongezeka
kwa Sh 17 kwa lita moja ya petroli sawa na asilimia 0.88, dizeli Sh 90
kwa lita sawa na asilimia 5.24 na mafuta ya taa Sh 72 kwa lita, sawa na
asilimia 4.28 ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita.
Kwa
upande wa bei za jumla, Mkurugenzi Mkuu huyo alisema pia zimeongezeka
kwa petroli, dizeli na mafuta ya taa, ambapo bei mpya za jumla zitakuwa
Sh 16.56 kwa lita moja ya petroli sawa na asilimia 0.93, dizeli Sh 90.20
kwa lita sawa na asilimia 5.59 na mafuta ya taa Sh 72.29 kwa lita sawa
na asilimia 4.58 .
Ngamlagosi
alisema kuongezeka kwa bei hizo katika soko la ndani, kwa kiasi kikubwa
kumetokana na kuongezeka kwa bei katika Soko la Dunia, na gharama za
usafirishaji wa bidhaa hiyo kuja nchini.
Pamoja
na mabadiliko hayo yanayoihusu nchi nzima, alisema bei hizo mpya,
hazitauhusu mkoa wa Tanga ambapo vituo vya mafuta mkoani humo vimeagizwa
kutopandisha bei mwezi huu.
Alisema
hatua hiyo inatokana na mkoa huo, kutokupokea mafuta mapya mwezi Julai,
na kufanya bei za Agosti kuendelea kutumika kama ilivyokuwa kwa mwezi
Julai.
“Mamlaka
(Ewura) inapenda kuukumbusha umma kwamba bei kikomo za mafuta kwa eneo
husika, zinapatikana vilevile kupitia simu za mkononi kwa kupiga namba
*152*00# na kisha kufuata maelekezo, ambapo huduma hii ni bure na
inapatikana kupitia mitandao yote ya simu za mkono nchini,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya Mwaka 2015, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko.
Alisema Ewura itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta na kuongeza; “ Taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta.”
Alisema
kampuni za mafuta, zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei
ya ushindani, mradi tu bei hizo ziwe chini ya bei kikomo, kama
ilivyokokotolewa na fomula iliyopitishwa na Ewura.
Alisema
vituo vyote vya mafuta, vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta
katika mabango, yanayoonekana bayana na yakionesha bei ya mafuta,
punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo
husika.
“Pale
ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za
mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei ndogo zaidi ili
kuhamasisha. Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei
inayoonekana vizuri kwa wateja,” alisema.
Mkurugenzi
Mkuu huyo alisema adhabu kali, itatolewa kwa kituo husika kwa
kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika. Alishauri
wanunuzi kuhakikisha kuwa wanapata stakabadhi ya malipo, inayoonesha
jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.
Alisema
stakabadhi hiyo ya malipo, itatumika kama kidhibiti cha mnunuzi wa
mafuta, endapo kutajitokeza malalamiko au kuuziwa mafuta kwa bei ya juu
kuliko bei kikomo ; au atauziwa mafuta yenye kiwango cha ubora
kisichofaa.
Sign up here with your email