WIZARA
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewataka wananchi
na wadau kutoa taarifa, iwapo kuna mashirika yasiyo ya kiserikali
(NGOs) zinazojihusisha na kuhamasisha vitendo vya ushoga nchini ili
hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya taasisi hizo.
Agizo
hilo lilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Msajili wa NGOs, Marcel
Katemba. Alisema kuwa siku za hivi karibuni, kumekuwepo na tuhuma za
kuwepo kwa baadhi NGOs kujihusisha na kuhamasisha vitendo vya ushoga
nchini.
Alisema
ni vyema jamii ikatambua kuwa NGOs zinasajiliwa kwa lengo la kutekeleza
majukumu yanayokubalika kisheria na kwamba vitendo vya kuhamasisha
ushoga si majukumu halali yanayopaswa kutekelezwa.
“Tunazitaka
NGOs kutekeleza majukumu yaliyo ndani ya usajili wao na kuepuka vitendo
vya uvunjifu wa sheria kwani kinyume na hayo hatua zitachukuliwa,” alisema Katemba na kusisitiza kuwa vitendo vya ushoga havikubaliki nchini kwani ni kinyume na mila, desturi na sheria za nchi.
Alisema
katika kudhibiti uwepo wa vitendo hivyo, wadau na umma kwa ujumla
wanapaswa kutoa taarifa zitakazowezesha kuthibitisha tuhuma hizo ili
hatua kali zichukuliwe kwa wahusika.
Katemba
alisema taifa lina mila, desturi na sheria za nchi ambazo imekuwa
ikizisimamia na kuzitekeleza na kuhamasishwa kwa vitendo hivyo
kunakwenda kinyume na misingi, ambayo kwa namna moja vinaweza kuathiri
kizazi kwa kizazi.
Alisema
ni wakati sasa kwa kila NGO kusimamia utekelezaji wa majukumu yake kama
ilivyosajiliwa, kuongeza ushiriki wake kwa kutoa michango yao katika
kuleta maendeleo kwa jamii.
Alisema
taratibu za usajili wa NGOS chini ya sheria mashirika yasiyo ya
kiserikali namba 24 ya mwaka 2002, yameimarishwa vyema na kila shirika
linalokuwa limepata usajili ni muhimu kutekeleza yale yaliyokusudiwa ili
kuepuka taifa kuingia katika vitendo visivyostahili.
Sign up here with your email