WAZIRI NCHEMBE AWAONYA POLISI . - Rhevan Media

WAZIRI NCHEMBE AWAONYA POLISI .


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ameitaka Polisi kutotumia nguvu kubwa katika mambo yasiyokuwa na manufaa kwa wananchi ila nguvu hizo zitumike kupambana na biashara ya dawa za kulevya kwa maslahi mapana ya taifa.

Nchemba ameyasema hayo juzi wakati akifunga mafunzo ya awali ya polisi na uhamiaji, katika Shule ya Polisi Tanzania-Moshi, ambapo zaidi ya wanafunzi 3,000 walihitimu mafunzo hayo.

Alisema polisi ikifanya jitihada za kutokomeza biashara na matumizi ya dawa ya kulevya, kila Mtanzania kwa kabila lake, kwa rangi yake na imani yake atalipongeza jeshi hilo kwa kazi ambayo watakuwa wameifanya.

Alisema wananchi hawataweza kulipongeza jeshi hilo kama litatumia nguvu kubwa ya kupambana na masuala yasiyo na tija kwa wananchi, ambapo aliwataka wahitimu wa mafunzo hayo kutekeleza kwa vitendo yale yote waliyofundishwa kwa mujibu wa taratibu za jeshi hilo.

Nchemba pia ameliagiza Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua kali za kinidhamu kwa mujibu wa taratibu za jeshi hilo, askari Polisi wanaokiuka maadili ya utendaji kazi wao, ikiwa ni pamoja na askari wanaobambikia watu kesi, kupokea rushwa pamoja na kukamata raia kwa kutumia nguvu zisizostahili.

Alilaani pia tabia ya wananchi kujichukuliwa sheria mkononi kama vile kuua watu wasiokuwa na hatia kwa visingizio za imani za kishirikina, pamoja na sheria kutofuatwa kwa watuhumiwa.

Mkuu wa Shule ya Polisi Tanzania- Moshi, Matanga Mbushi, alisema wanafunzi hao wamepewa mafunzo mbalimbali yatakayowawezesha kufanya kazi kwa ufanisi na kuongeza kuwa kati ya wanafuzi wanaohitimu, wanafunzi 99 wametimuliwa kutokana na makosa ya nidhamu na mimba.

Previous
Next Post »