VYAMA 17 VYA SIASA KUADHIBIWA. - Rhevan Media

VYAMA 17 VYA SIASA KUADHIBIWA.

VYAMA 17 vya siasa nchini, viko hatarini kutumikia adhabu ya kutoshiriki uchaguzi nchini sambamba na kulipa faini ya Sh milioni tatu, baada ya kushindwa kuwasilisha ndani ya muda uliowekwa wa marejesho ya taarifa ya gharama za Uchaguzi Mkuu uliofanywa Oktoba 25 mwaka jana.
Hatua hiyo imekuja baada ya muda wa kuwasilisha taarifa za gharama hizo kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuisha jana saa 10 jioni, ambapo jumla ya vyama vitano ndivyo vilivyokuwa vimewasilisha taarifa zake.
Msajili Msaidizi wa Kitengo cha Gharama za Uchaguzi na Elimu kwa Umma, Piencia Kiure wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, alisema hadi juzi, ni vyama vitatu kati ya 22, ndivyo vilivyozingatia muda uliowekwa wa kupeleka taarifa ya gharama za Uchaguzi Mkuu uliopita.
Alivitaja vyama vilivyozingatia kuwa ni pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha ACT-Wazalendo na kuvitaka vyama vingine vihakikishe ifikapo Juni 25 (jana), viwe vimepeleka taarifa hiyo kwa kuwa ndiyo siku ya mwisho ya kuwasilisha.
Kiure alitaja adhabu kwa vyama vitakavyoshindwa kuwasilisha taarifa hiyo ndani ya muda uliowekwa ni kutozwa faini isiyozidi Sh milioni tatu na kutoruhusiwa kushiriki uchaguzi hadi watakapowasilisha taarifa hiyo.
Adhabu ya wagombea ambao hawajapeleka taarifa ni kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja au faini isiyozidi Sh milioni mbili au kutumikia adhabu zote kwa pamoja. Hata hivyo jana Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pamoja na Chama cha ADC, viliwasilisha taarifa zao za gharama hizo na kufanya idadi ya vyama hivyo kuwa vitano.
Akizungumza mara baada ya kuwasilisha taarifa hiyo kwa Ofisi ya Msajili, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, wa Chadema, Roderick Lutembeka alisema wametii Sheria ya Gharama ya Uchaguzi kama inavyoelekeza kwenye kifungu cha 18 cha sheria hiyo ya mwaka 2010.
Lutembeka alisema sheria hiyo inaagiza vyama vyote vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi mkuu kuwasilisha kwa Msajili wa Vyama gharama za uchaguzi na kwamba ofisi ya msajili nayo imeweka utaratibu wa kuwasilisha taarifa hizo, ambayo jana ndiyo ilikuwa siku ya mwisho.
“Tumetii agizo la sheria na tumewasilisha ndani ya muda uliopaswa, ila gharama tulizotumia tutazitaja baadaye, tuache kwanza msajili azione azifanyie kazi, ila hatukufikia kiwango cha mwisho cha gharama kwa mujibu wa matakwa ya sheria ya gharama za uchaguzi,” alisema Lutembeka.
Kwa upande wao Kamishna Mkuu wa Chama cha ADC, Doni Mnyamani alisema wamewasilisha taarifa ya gharama za uchaguzi kwa Msajili wa Vyama kwa wakati, ili kutekeleza matakwa ya sheria.
Previous
Next Post »