Picha na the Habari |
Dotto Kahindi
Kilimo na ufugaji usioendelevu, uchimbaji wa madini na
ukataji wa miti kwa matumizi ya kuni, mkaa na ujenzi ni mambo makuu matatu adui
wa mazingira ambayo yanakwamisha jitihada za serikali na asasi mbalimbali katika
kukabiliana na uharibifu wa mazingira
Mambo hayo yameainishwa hivi majuzi na
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho ya siku ya mazingira
dunia, jambo ambalo linatoa fursa kwa serikali na wadau kwa ujumla kuweka nguvu
zao katika kukabiliana na mambo hayo adui wa mazingira.
Kumjua adui yako ni hatua moja katika
kujihakikishia ushindi wa vita, jambo la pili na muhimu ni kujua silaha za huyo
adui yako ili iwe rahisi kwako kuandaa silaha zenye maangamizi kumshinda yeye
wakati jambo la tatu ni kuweka mikakati madhubiti ya namna ya kutoa
mashambulizi
Samia anataja njia kadhaa za
kukabiliana na maadui hao ikiwemo kuundwa kwa kamati za mazingira kuanzia ngazi
za vijiji, vitongoji, mitaa, kata na wilaya zitakazosimamia vyanzo vya maji
vilivyopo katika maeneo yao.
Bila shaka Mama Samia anataarifa za
kutosha kwamba mbinu na silaha hizi zitafanikisha kupunguza kama si kukomesha
kabisa uharibifu wa mazingira hasa kwenye vyanzo vya maji kama kauli mbiu ya
maadhimisho ya siku ya mazingira ya mwaka huu ambayo inahimiza uhifadhi wa vyanzo
vya maji kwa uhai wa taifa letu.
Tanzania iliamua kuwa na kauli mbiu
tofauti na ile ya kimataifa ambayo inasema `Go Wild For Life' ujumbe ambao unahamasisha
kuchukua hatua za kulinda maisha ya wanyamapori kwa kuwa wanaunda sehemu muhimu
ya mazingira.
Hii ni kutokana na uharibifu mkubwa wa
vyanzo vya maji hapa nchini ambao umesababisha kupungua kwa mtiririko wa maji
katika mito ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, baadhi ya mito
imebadilika na kuwa ya msimu, kuchafuliwa na hata mingine kukauka.
Samia akasema uchafuzi wa mazingira wa
vyanzo vya maji kama vile Rufiji, Pangani, Ruaha ukiendelea, huenda itakauka
ndani ya miaka 15 ijayo na hivyo kuhimiza upandaji wa miti kwenye maeneo
yanayozunguka vyanzo hivyo na kupiga marufuku shughuli zinazoviharibu.
Vizuri tumewajua maadui japo kwa
kuchelewa, lakini tunahitaji kushirikisha wadu na mamlaka mbalimbali kupima
uwezo wao, ili tuweze kuandaa silaha na mikakati madhubuti ya kupamnana nao na
hatimaye kunusuru vyanzo vyetu vya maji.
Sign up here with your email