Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limepokea taarifa juu ya mpango na
kauli za baadhi ya viongozi wa Young Africans SC kushawishi mashabiki
wao kufanya vurugu dhidi ya warushaji matangazo ya televisheni ya moja
kwa moja wakati wa mchezo wa Kombe la Shirikisho la Afrika ngazi ya
Makundi kati ya Young Africans ya Tanzania na TP Mazembe ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC) utakaofanyika Juni 28, 2016 saa 10.00 jioni
kwenye Uwanja wa Dar es Salaam.
TFF
ikiwa msimamizi mkuu wa mpira wa miguu Tanzania, inawajibika na mara
moja inachukua nafasi hii kuwatahadharisha baadhi ya viongozi wa Young
Africans, wanachama na mashabiki wao kutofanya hivyo kwani itakuwa ni
kinyume na kanuni za mashindano na mikataba ya udhamini katika hatua
hii.
Ikumbukwe
kwamba CAF inamiliki asilimia mia moja ya haki za habari na masoko
katika ngazi hii ya makundi na jaribio lolote la kukwamisha matangazo ya
biashara au utengenezaji na urushaji wa matangazo ya televisheni au
ukwamishaji wa shughuli zingine kama hizo kwa CAF au wakala aliyeteuliwa
na CAF kutaigharimu klabu mwenyeji si kwa kutozwa faini tu lakini pia
uwezekano wa kuondolewa mashindanoni.
Pia
TFF inatoa tahadhari hiyo ikiwamo ile ya utamaduni wa kukaa uwanjani
ili kuepusha aina yoyote ya vurugu kwenye michezo yake hususani hii ya
hatua ya makundi. TFF inafahamu kuwa tayari viongozi wa Young Africans
walikwisha kusoma nyaraka na taarifa mbalimbali kuhusu kanuni na masuala
ya udhamini kwa timu zinazofuzu hatua ya Nane Bora.
Wapenzi
wa Yanga wanaombwa kufika kwa wingi na kuishangilia kwa nguvu timu yao
ikiwa ni njia ya kuitia hamasa.Hata hivyo shamrashamra hizo zifanyike
kwa kufuata sheria,kanuni na taratibu za Mpira wa Miguu na sheria za
nchi.
Vitendo
vya kuashiria vurugu na kufanya vurugu vikithibitishwa katika taarifa
ya Mwamuzi, Janny Sikazwe wa Zambia; Kamishna wa mchezo, Celestin
Ntangungira wa Rwanda na Mratibu Mkuu Maalumu kutoka Msumbiji, Sidio
Jose Mugadza, hatua zake zitachukuliwa dhidi yake ikiwamo KUONDOLEWA
KWENYE MASHINDANO. Vilevile vitendo vya kutishia amani,kudhuru mwili au
kuharibu mali vitachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za kijinai.
Katika
mchezo huo wa kimataifa Na. 107, Mwamuzi Sikazwe atasaidiwa na Jarson
Emiliano dos Santos kutoka Angola atayekuwa kwenye mstari wa kulia (line
1) na Berhe O’Michael wa Eritrea atayekuwa upande wa kushoto (line 2)
huku Wellington Kaoma wa Zambia akiwa ni mwamuzi wa akiba.
Wakati
huohuo, kikao cha Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
nchini kinatarajia kukaa siku ya Jumamosi tarehe 2 Julai 2016. Taarifa
zaidi itatolewa karibuni.
Sign up here with your email