Maalim Seif arejea nchini, azungumzia ripoti ya NEC
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliwasili mjini hapa jana baada ya kumaliza ziara ya kichama katika mataifa mbalimbali ya Magharibi.
Katika
ziara ya takriban wiki mbili, Maalim Seif na ujumbe wake akiwamo
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Ismail Jussa Ladhu, walitembelea
Canada, Marekani na Umoja wa Mataifa, jijini New York.
Maalim
Seif aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume, Kisauni
mjini hapa saa 11 za alasiri na kupokewa na viongozi mbalimbali
wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui.
Katika
salamu zake fupi, Maalim Seif alisema ripoti ya uchaguzi
iliyowasilishwa juzi kwa Rais John Magufuli na Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) haiwezi kuwa na jawabu la mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar, kwani
waliosaidia kuuvuruga ndio walewale waliojidai kuwasilisha ushahidi,
jambo ambalo haliwezi kukubalika.
Alisema
tatizo la Zanzibar bado lipo na dawa yake ni kuirejesha haki ya
kidemokrasia ya wananchi walioamua kupitia masanduku ya kura ya Oktoba
25, 2015.
“Hili,
chama cha CUF kilikwishalitolea maamuzi kupitia maazimio ya Baraza Kuu,
kama mnakumbuka, nayo ni pamoja na kutoitambua Serikali ya Dk Shein na
kuendelea kuikataa kwa vitendo na nafsi na pia kuendelea kudai haki ya
maamuzi ya wananchi hadi pale itakapopatikana,” alisema.
Makamu
huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar katika Serikali iliyopita alisema;
“kwa hili watawala wasijisumbue, wananchi hawajalala na katu hawatorudi
nyuma, wewe wacha watoe tu hizo ripoti zao... msimamo wetu upo
palepale”.
Kuhusu
ziara yake, Maalim Seif alisema ilikuwa ya matumaini na mafanikio
makubwa katika kufanikisha juhudi za kutetea na kupigania haki ya
kidemokrasia ya wananchi na kwamba muda ukifika ataweka bayana zaidi
mafanikio hayo.
Katika
ziara hiyo Maalim Seif aliwasilisha mada ya ‘Chaguzi za Zanzibar: Haki
iliyocheleweshwa’, katika mkutano wa kimataifa ulioandaliwa taasisi za
kimataifa za taaluma za siasa, stratejia na demokrasia za NDI, IRI na
CSIS za Marekani
Sign up here with your email