TANZANIA ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazopiga hatua kubwa mbele kuwekeza kwenye sekta ya elimu katika nchi zinazoendelea kusini mwa jangwa la Sahara.
Serikali imejitahidi sana kuweka fursa ya kuwawezesha vijana wengi nchini kupata elimu, pia kuwezesha sekta binafsi nazo kutoa elimu kupitia shule na vyuo binafsi.
Kuanzishwa kwa shule za kata wakati wa utawala wa rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, kulitanua wigo mpana kwa wanafunzi wengi nchini kujiunga na elimu ya sekondari nchini kwa gharama nafuu.
Kuongezeka kwa idadi kubwa ya wanafunzi kujiunga na elimu ya sekondari nchini kulisababisha pia ongezeko la idadi kubwa ya wanafunzi kujiunga na elimu ya juu nchini hali iliyosababisha kuanzishwa kwa vyuo vikuu zaidi nchini vya serikali na binafsi.
Ni wakati huu ndipo Chuo Kikuu cha Dodoma kilianzishwa ikisemekana ndicho chuo kikubwa zaidi Afrika kikiwa na uwezo wa kuhimili wanafunzi elfu arobaini. Vilevile paliongezeka vyuo vingine vya kidini kama vile Saint John na Saint Augustine cha Jijini Mwanza kikijipanua zaidi kwa kuongeza matawi mikoani.
Lengo kuu la kuanzishwa kwa kwa vyuo hivi ilikuwa kuwezesha idadi kubwa ya wanafunzi kujiunga na elimu ya juu nchini, huku wakisapotiwa kwa asilimia kubwa na serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya elimu ya juu nchini (HESLB). Kwa asilimia kubwa lengo hili lilifanikiwa kwa wanafunzi wengi wenye sifa kujiunga na elimu ya juu nchini.
Maada ya leo ni kujikita zaidi katika kuchambua na kudadavua maisha ya wanachuo walio wengi nchini baada ya kuhitimu elimu yao. Ni juu ya uhalisia wa maisha ya vijana wengi nchini kwa sasa baada ya kuhitimu kwao.
Michezo ya kubahatisha (betting)
Wengi wa wanachuo waliomaliza vyuo ambao hawapewi ajira ya moja kwa moja na serikali wamejiingiza katika michezo ya kubahatisha ambayo kamari inayoendeshwa kisasa kupitia mashine maalum au simu za mkononi.
Idadi yao inazidi kuongezeka hasa maeneo ya mjini ambako wasomi wengi hukimbilia kwa kile wanachokiamini watapata ajira kwa urahisi.
Kazi mbadala
Wanachuo wengi waliopo mtaani wanajihusisha na kazi tofauti na kile walichokisomea. Mmoja wa wanafunzi hao hivi sasa amekuwa dalali wa magari ili aweze kupata riziki yake ikiwa ni tofauti kabisa na kile alichokisomea chuoni, yaani shahada ya uhusiano wa kimataifa. Mwingine ni mwalimu wa masomo ya ziada ‘tution’ kazi ambayo ni tofauti kabisa na masuala ya uchumi aliyosomea chuoni.
Utegemezi
Vijana wengi waliomaliza elimu ya juu bado ni tegemezi kutokana na ukweli kwamba hakuna ajira za moja kwa moja toka serikalini za kuweza kuwaajiri wanachuo wote, hali inayosababisha wengi wao kuendelea kuwa tegemezi.
Mwanafunzi mhitimu mwingine wa karibu alimaliza chuo kikuu toka mwaka 2013 akifaulu vyema katika masomo ya uhifadhi mazingira lakini mpaka sasa bado anawategemea wazazi wake pamoja na umri wake mkubwa wa miaka 32.
Kujikita katika uhalifu wa mtandao
Zamani ilikuwa ni kitu cha ajabu kwa kijana msomi nchini kukamatwa kwa masuala ya wizi ama utapeli wa aina yoyote. Ilionekana mwizi au kibaka ni yule asiye na elimu. Hivi sas hali imekuwa tofauti, vijana wengi wamekuwa wezi kwa njia ya mtandao na baadhi kutumia elimu yao kujifanya maofisa wa serikali ili watimize dhamira yao.
Biashara ya umalaya
Hili ni janga kubwa zaidi nchini kwa sasa likiwaathiri zaidi watoto wa kike ambao walizoea maisha ya chuo kupewa pesa na serikali baada ya kumaliza chuo na kukosa ajira baadhi yao wamejiingiza kwenye biashara ya kuuza miili yao kwa watu wenye pesa ili wakidhi mahitaji yao muhimu.
Kushamiri kwa rushwa ya ngono
Ukosefu wa ajira nchini umepelekea kushamiri kwa kasi rushwa ya ngono na wahanga wakubwa wamekuwa ni watoto wa kike. Viongozi wengi hasa wenye nafasi au dhamana ya kuajiri wanatumia mwanya huo kuwarubuni watoto wa kike wenye uhitaji wa kazi kwa kisingizio cha kuwapa ajira wakitimiza masharti yao.
Wengi ni wahanga wa suala hili hali inayopelekea kuenea kwa kasi kwa maambukizi ya UKIMWI na wengine kupata msongo wa mawazo na kuathirika kisaikolojia.
Vijana wa kiume kulelewa na wanawake matajiri
Huu ni mchwa mwingine mkubwa unaomaliza kizazi cha sasa cha vijana wasomi ambao kulingana na ugumu wa maisha wengi wao wanalelewa na akina mama wenye pesa akipewa kila kitu na yeye kumtimizia mahitaji yake ya ngono.
Huu ni utumwa wa mapenzi ambapo vijana wengi wanaingia kwa kukosa pesa au mahitaji muhimu bila kujali afya zao.
Rafiki yangu mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe mtandaoni, aliwahi kuthibitisha akisema: “Kaka ni kweli nipo na mama… kanipa gari na nyumba na kila siku analala kwangu, kuhusu afya sijali liwalo na liwe!” Kauli hii inathibitisha namna gani ugumu wa maisha unaua ndoto za vijana wengi.
Mzigo wa madeni
Pamoja na wengi wao kuamua kupambana na maisha ili waweze kusimama wenyewe kikwazo kikubwa kinakuwa mitaji hali inayowalazimu kuingia kwenye mikopo yenye riba kubwa na baadaye kujikuta wakiingia kwenye madeni makubwa.
Dada mmoja (jina linahifadhiwa) aliwahi kusema: “Kaka mimi nimekopa kwenye kikundi shilingi laki mbili na natakiwa kurudisha elfu kumi kila siku kwa siku thelathini”, maana yake amekopa laki mbili na atatakiwa kurejesha laki tatu.
Pamoja na kuwa hana ajira lakini deni lake alilokopeshwa na serikali wakati yuko chuo kadri muda unavyozidi kusonga mbele ndivyo riba inazidi kuongezeka.
Kutoaminiwa na taasisi za fedha
Taasisi nyingi za kibenki nchini haziwakopeshi vijana wasio na ajira au dhamana isiyohamishika kama nyumba, shamba au hati ya kiwanja.
Kilio cha vijana wengi kiko hapa kwa maana hakuna taasisi ya kibenki iliyo tayari kumkopesha mtu bila kuwa mwajiriwa au kuwa na dhamana inayokubalika, hivyo wengi wao kukimbilia kwenye SACCOS zenye riba kubwa zisizo rafiki.
Ni ukweli usiopingika kuwa vijana wengi waliomaliza elimu ya juu wanapitia kipindi kigumu sana kwenye maisha yao kwa sababu ya tatizo sugu la ukosefu wa ajira nchini. Hivyo ni jukumu la kila Mtanzania mwenye uwezo au njia mbadala ya kuelekeza ni namna gani tunaweza kuwasaidia vijana wetu na hatimaye kuondokana na tatizo sugu la uhaba wa ajira.
Sign up here with your email