WAASI WA UGANDA WASHAMBULIA MASHARIKI MWA DRC. - Rhevan Media

WAASI WA UGANDA WASHAMBULIA MASHARIKI MWA DRC.

Watu kadhaa wameuawa na kujeruhiwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya waasi wa Uganda kufanya mashambulizi kwenye maeneo hayo.

Mtandao wa habari wa Africa Time umezinukuu duru za kijeshi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zikitangaza kuwa, wanajeshi wawili wa nchi hiyo waliuawa jana Jumanne baada ya waasi wa ADF wa Uganda kufanya mashambulizi katika mji wa Opita, kaskazini mwa mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa Kongo na wanajeshi wengine wanne wamejeruhiwa. 

Hata hivyo duru hizo hazikusema chochote kuhusu hasara walizopata waasi katika mapigano hayo.

Waasi wa Uganda wanaoipinga serikali ya Rais Yoweri Museveni wako mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu mwaka 1995 hadi hivi sasa. Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Kongo pamoja na serikali ya nchi hiyo wanaamini kuwa waasi hao wa Uganda wamefanya mauaji ya raia 550 katika eneo la Beni huko Kivu Kaskazini tangu mwezi Oktoba 2014 hadi hivi sasa.

Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetumbukia kwenye machafuko na mashambulio ya waasi kwa miaka 20 sasa. Jeshi la Kongo pamoja na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa hadi sasa wameshindwa kudhibiti vitendo hivyo vya waasi na kuwaletea amani na usalama wakazi wa maeneo hayo.
Previous
Next Post »