UKAWA WAMVAA SPIKA NDUGAI. - Rhevan Media

UKAWA WAMVAA SPIKA NDUGAI.

WABUNGE wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamemtaka Spika wa Bunge, Job Ndugai, akubali kwanza kuwapo maridhiano ya wapinzani kuchagua viongozi wa kamati mbili muhimu,


ambazo hazina wenyeviti kwa miezi kadhaa sasa.
Mkutano wa Tatu wa Bunge unaanza leo mjini Dodoma, huku Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), zikiwa hazina wenyeviti, tangu kufanyika kwa uchaguzi wa Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge, Januri 21, mwaka huu.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia, ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), alisema kwa mujibu wa Kanuni za Bunge la Tanzania, kamati hizo ni lazima ziongozwe na wapinzani na kwamba wanaingia bungeni leo, wakiwa na ushauri wa kutaka kuitishwa meza ya mazungumzo kwa ajili ya maridhiano.
Mbatia alizungumza Nipashe jana wilayani Hai, Kilimanjaro, baada ya kumaliza maziko ya Luteni Kanali Mstaafu Maxmillan Mbowe (65), ambaye ni kaka wa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungune na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, aliyezikwa kijijini kwao, Nshara, Machame.
Mbatia alisema: “Kwanza lazima wenzetu wa upande wa pili wajue kwamba hizi ni kamati zenye jukumu la kusimamia vizuri matumizi ya umma kwa niaba ya Watanzania, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge," alisema.
Aliongeza kuwa: "Rai yetu kwa Mheshimiwa Spika, akubali tuwe na meza ya maridhiano ili tuone njia gani bora tunayoweza kuitumia kupata viongozi kutoka ndani ya wapinzani, badala ya hii mivutano inayoendelea, ambayo haina tija katika ustawi wa demokrasia na ukuzaji wa usimamizi wa rasilimali za taifa hata kwa uimara wa Bunge.”
Kutokana na mvutano huo, wapinzani wamemtaka pia Spika Ndugai kukutana na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kutafuta ufumbuzi kuhusu namna bora ya kuwapata wenyeviti hao na kuondoa mvutano uliopo, kwa afya ya muhimili wa Bunge.
Wakati wabunge hao wakikomalia kuruhusiwa kupendekeza majina ya viongozi wa kamati hizo, Ukawa itakutana na wabunge wote leo mjini Dodoma kwa ajili ya kukubaliana masuala ya msingi watakayoyasimamia katika kipindi chote cha Bunge la Bajeti kwa mwaka 2016/2017.
“Tumesema masuala mengine yote ambayo tutayasimamia bungeni katika Bunge hili la Bajeti tutayatolea ufafanuzi kwa kuyaeleza kwa ufasaha, baada ya kikao cha kesho (leo) cha wabunge wote wa Ukawa,” alisema Mbatia.
Wakati wapinzani wakitaka kupewa fursa ya kuongoza kamati hizo kwa wenyeviti watakaowapendekeza, bado kuna utata wa chama gani kiongoze Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), ambayo imepewa jukumu la kukagua hesabu za mashirika ya umma.
Kwenye mkutano huo wa Bunge, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), anatarajia kuwasilisha ripoti yake ya mwaka uliopita ambayo hukabidhiwa kwa kamati hizo mbili.
MAZISHI YA KANALI MBOWE
Katika mazishi hayo ya Kanali Mbowe, yaliyoongozwa na Mkuu wa Jimbo la Hai la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Mchungaji Aminirabi Swai, viongozi mbalimbali wa kitaifa walitoa salamu za rambirambi, akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadick.
Wengine waliohudhuria ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Limited, Dk. Regnald Mengi, Katibu Mkuu wa Chadema Taifa, Dk. Vincent Mashinji, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa na Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania, Edwin Mtei.
Katika mazishi hayo yalihudhuriwa pia na wabunge wa vyama mbalimbali, waliwakilishwa na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
Kanali Maxmillan Mbowe alifariki dunia Aprili 13, mwaka huu, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa akipatiwa matibabu
.
Previous
Next Post »