MOTO WATEKETEZA MADUKA NA VIBANDA KAGERA. - Rhevan Media

MOTO WATEKETEZA MADUKA NA VIBANDA KAGERA.

MADUKA 34 na vibanda vya mbao 83 katika Soko la Kayanga lililoko katika Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, yameteketea kwa moto uliozuka ghafla na kusababisha hasara kubwa.

Moto huo ulizuka mwishoni mwa wiki majira ya saa 1:30 usiku ukianzia katika moja ya kibanda cha mbao na baadaye kusambaa katika vibanda jirani vya mitumba, viatu na bidhaa nyingine.
Baadhi ya wananchi wa eneo hilo walijitahidi kuokoa mali zao kwa kuvunja vibanda vya biashara.
Hata hivyo, moto huo uliwazidi nguvu wananchi na kuendelea kuwaka kwa kasi zaidi na kusambaa katika maduka yaliyopo magharibi mwa soko la Kayanga na kuanza kuyaunguza maduka.
Uongozi wa Wilaya ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Deodatus Kinawiro, ulifika katika eneo la tukio usiku huo na baadaye kuomba msaada wa zimamoto kutoka mjini Bukoba.
Kikosi cha Zimamoto cha mjiji Bukoba kiliwasili mjini Kayanga usiku huo na kukuta moto huo ukiwa tayari umeteketeza baadhi ya maduka na vibanda hivyo.
Hata hivyo, kikosi hicho kwa kushirikiana na Kikosi cha Zimamoto Karagwe, walifanikiwa kuudhibiti moto huo usiendelee na kufanikiwa kuuzima saa 8:30 usiku.
Kadhalika, Kamanda wa Polisi Mkoa Kagera, Augustine Uromi, alikuwapo eneo la tukio usiku huo.
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Kinawiro alisema maduka 34 kati ya 112 yalipo sokoni humo, yameteketea kwa moto huo.
Pia alisema vibanda 83 kati ya vibanda 135 vinavyozunguka soko hilo, vimeungua.
Aidha, Kinawiro aliwapa pole wote waliounguliwa na maduka na vibanda pamoja na mali zao.
Pia aliwatahadharisha waliopora mali katika tukio hilo kuzirejesha kwa kuwa huo siyo moyo wa kiungwana.
Vile vile, aliwataka wanaookota mabaki ya bidhaa zilizosalia katika tukio hilo kwa malengo ya kwenda kuzitumia, kuacha mara moja kwa kuwa kufanya hivyo ni hatari kula vitu vya sumu na kupata madhara.
Chanzo cha moto huo mpaka hakijajulikana pamoja na thamani ya mali zilizoteketea na uchunguzi unaendelea.
Previous
Next Post »