MAYANGA AMWAGA LAWAMA KWA MAREFA. - Rhevan Media

MAYANGA AMWAGA LAWAMA KWA MAREFA.


WAKATI Kocha wa Simba, Jackson Mayanja akiomba radhi mashabiki na wanachama wa klabu hiyo pamoja na kumshushia lawama mwamuzi wa mchezo wao wa kipigo cha goli 1-0 dhidi ya Toto African,

uongozi wa klabu hiyo umepanga kukutana kufanya tathmini ya mwenendo wa timu hiyo kuelekea kwenye michezo mitano ya iliyobakia.
Rais wa Simba, Evans Aveva alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa watakutana haraka na kuweka mikakati kuhakikisha hawapotezi pointi kwenye michezo hiyo.
"Ni matokeo ambayo tayari yameshatokea, kwa sasa tunaangalia mbele na tutakutana kupitia ripoti ya kocha ya michezo hii miwili tuliyopoteza ili tujipange upya kupambana," alisema Aveva.
Wakati Aveva akisema hayo, Kocha Mayanja amesema kwamba anawaomba radhi wanachama na mashabiki wa Simba kufuatia kipigo ambacho timu hiyo imepata.
Mayanja alisema kuwa matokeo hayo ya juzi yameharibu mbio za kusaka ubingwa wa Bara kama ambavyo walikuwa wanatarajia kuuchukua kutoka kwa mahasimu wao msimu huu.
Kocha huyo aliongeza kuwa refa Hamada Simba kutoka Kagera alichezesha mechi hiyo chini ya kiwango mchezo huo na kupelekea kufanya makosa yaliyoigharimu timu yake.
Mbali na kuomba radhi, Mayanga amelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupanga waamuzi wenye beji za FIFA katika michezo inayohusisha Simba, Yanga na Azam FC ili watakapoboronga watakutaka na adhabu kutoka katika shirikisho hilo linalosimamia mchezo huo duniani.
Alishangazwa pia na uamuzi wa kumtoa kwenye kwenye la ufundi la timu hiyo na akakanusha kutoa lugha ya matusi kwa refa huyo wa kati kama ilivyodaiwa.
"Sijawai kutukana refa katika maisha yangu, nilimwambia aangalie vitendo wanavyofanyiwa wachezaji wangu., na hili hata kwa wenzetu Ulaya tunaona makocha wanazungumza na marefa endapo anaona mambo hayaendi sawa, huku kwetu ukimsemesha refa anakuadhibu, inashangaza sana," alisema Mayanja.
Hata hivyo Mayanja ambaye ajira yake imekalia kuti kavu alisema kuwa pamoja na kufungwa kwenye mchezo wa juzi bado hawajakata tamaa na watapambana hadi mechi ya mwisho ya kufunga pazia la ligi hiyo.
"Mpira ni mchezo wa makosa uwezi kujua nini kitatokea kesho, " Mayanja alisema.
Simba iliyocheza mechi 25 iko katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 57 wakati mahasimu wao Yanga wenye mchezo mmoja pungufu wako kileleni wakiwa na pointi 59 huku Azam FC ikifuatia baada ya kufikisha pointi 55.
Previous
Next Post »