TFDA YACHOMA VIROBA TANI 8. - Rhevan Media

TFDA YACHOMA VIROBA TANI 8.


MAMLAKA ya Mapato (TRA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) zimeteketeza viroba vya pombe inayoingizwa kutoka Uganda na vipodozi, vilivyokamatwa wilayani Missenyi kutokana na oparesheni mbalimbali.


Akizungumza baada ya kuteketeza bidhaa hizo katika eneo la Mwisa, Afisa wa TRA mkoa wa Kagera, Jeston Kamola alisema bidhaa zilizokamatwa na kuteketezwa zina uzito wa tani nane na kuwa thamani yake ni zaidi ya Sh. milioni 28.9.
Kamola alitaja bidhaa zilizoteketezwa kuwa ni viroba aina ya Vodka na Empire ambavyo kisheria haviruhusiwi kwa matumizi ya binadamu nchini.
Alisema viroba hivyo vilikamatiwa katika maeneo ya Bugabo vikiingizwa kwa njia ya maji kutoka Uganda, na vipodozi ambavyo vimekwisha muda wake vilivyokutwa katika stoo za wafanyabiashara.
“Tunapokamata bidhaa kama hizi, ambazo zitaonekana ziliingizwa kinyemela lakini zinastahili kulipiwa kodi, tunachukua chombo kilichokutwa nazo, tunawatoza faini na kutakiwa kulipa kodi inayotakiwa," alisema Kamola.
"Lakini zikikamatwa (bidhaa) za vyakula visivyoruhusiwa, tunaomba watuonyeshe vibali vya TFDA na mamlaka nyingine kama hawana, vinateketezwa.
” Afisa wa TRA mkoa huyo aliwataka wananchi kutopenda kutumia bidhaa za nje wakati zipo bidhaa za ndani ambazo zina ubora unaotakiwa. Aidha, aliwataka wafanyabiashara kutopenda kutumia njia za mkato, na badala yake wazihusishe mamlaka husika ili kuepuka kupata hasara na kupoteza mitaji yao.
Naye mratibu wa TFDA wilaya ya Missenyi, Justina Mgabe alisema kuwa wilaya hiyo iko mpakana na ndiyo maana imekuwa ikiathiriwa sana na bidhaa kutoka nje ya nchi zikiwamo zilizopigwa marufuku.
Mgabe alisema wanafanya kila jitihada kuhakikisha maafisa wa TFDA walio mipakani wanafanya ukaguzi kwa magari yote ya mizigo yanayopita maeneo hayo kuingia nchini ili kukamata bidhaa zisizo halali.
Naye Afisa Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, Zablon Segeru aliwataka wananchi, hasa vijana kuacha kutumia bidhaa zisizo na ubora, zilizopigwa marufuku au zilizokwisha muda wake maana zina madhara makubwa kwa afya zao.
“Vijana wakinywa viroba mfano Vodka ina kilevi asilimia 44! Kina madhara makubwa maana kitadhoofisha mwili na kumfanya kushindwa kufanya shughuli za maendeleo," alisema Segeru.
Previous
Next Post »